
Mpango wa Uingereza ulikusudia kuanzisha serikali ya ndani ya Wayahudi, chini ya uangalizi wa koloni. Baraza hilo lingesimamia miundombinu, elimu na polisi, lakini bado likiwa chini ya uangalizi wa wakoloni Waingereza.
Wazungu waliokuwa wamekwisha weka makazi Afrika Mashariki walipinga vikali. Magazeti ya kikoloni yaliandika makala kali dhidi ya mpango huo, wakikiita “Jewganda”. Wazungu walikutana Nairobi na kutishia vurugu iwapo mpango huo ungefanywa.
Herzl alijadiliana kwa miezi kadhaa kabla ya kuwasilisha pendekezo hilo kwenye kongamano la Uzayuni Agosti 1903. Hakutarajia kuwa pendekezo hilo lingevunja umoja wa harakati hizo.
“Wanachama wa kongamano la Uzayuni walikataa Mpango wa Uganda, wakisisitiza kwamba Palestina ni nchi yao,” asema Dr Serhat Orakçı kutoka Chuo Kikuu cha Haliç, Uturuki.
Wengine waliona Afrika kama hifadhi ya muda, lakini wengi walikataa.
“Wangewezaje kukubali ardhi ya isiyojulikana ya Afrika ilhali ndoto yao ya kale ilikuwa Zion (Yerusalemu)? Kufikia 1905, mpango huo ulikufa,” asema Şanlı.
Ndoto zinazoendelea
Mpango wa Uganda ulitangulia Azimio la Balfour la 1917, ambalo Uingereza iliahidi kusaidia kuanzisha makazi ya Wayahudi Palestina. Lakini hata baada ya azimio hilo, juhudi za kutafuta ardhi Afrika kwa ajili ya Wayahudi ziliendelea.
“Angola ilitajwa, lakini Ureno – mkoloni wa eneo hilo – ilikataa. Mpango wa Madagascar ukajadiliwa miaka ya 1930, lakini haukutekelezeka. Mwaka 1944, Ethiopia ilijadiliwa, lakini Mfalme Haile Selassie alikataa – japo Ethiopia ilikuwa na jamii ya Wayahudi wa Beta Israel,” asema Şanlı.
“Kwa hivyo, kila mpango uligonga mwamba – mara nyingine Wayahudi wenyewe walikataa, na mara nyingine wakoloni walikataa. Katika kesi ya Ethiopia, taifa hilo huru lilikataa kabisa”.
Mpango mpya?
Baada ya mashambulizi ya Hamas tarehe 7 Oktoba dhidi ya Israel, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amekuwa wazi kuhusu nia ya kuifuta Gaza kwa madai ya kulipiza kisasi.
Nchi kadhaa za Afrika – ikiwemo Sudan, Somalia, Sudan Kusini na Uganda – zinatajwa kuwa maeneo yanayopendekezwa kuhamishia Wapalestina waliopoteza makazi, japo serikali zao zinakanusha kuhusika na mpango huo.
Viongozi wa siasa kali nchini Israel wamekuwa wakitaka Wapalestina wafukuzwe kabisa ili kuruhusu upanuzi wa makazi ya Wayahudi Gaza.
Historia inajirudia
Wataalamu wanasema kuwa hali hii inaonesha mtazamo wa kikoloni unaoendelea, ambapo Afrika huchukuliwa kama ardhi tupu ya kupeleka watu wasiotakiwa kwingineko.
“Zaidi ya miaka 100 iliyopita, Afrika ilichukuliwa kama mahali pa kuwaweka Wayahudi. Sasa, tunasikia pendekezo la kuwapeleka Wapalestina huko. Mantiki hiyo hiyo bado ipo. Kwa Ulaya, na sasa Israel, Afrika huonekana kama sehemu ya kutupa matatizo yao,” asema Şanlı.
“Mipango hii inazungumzia zaidi kuhusu Ulaya na Israel – siyo Afrika.”
Mwanachuoni kutoka Afrika Kusini, Jo Bluen, ambaye alisaini barua ya wanasayansi 800 Novemba 2023 iliyotangaza matendo ya Israel kuwa ya mauaji ya halaiki, anataka Afrika ichukue hatua kali zaidi dhidi ya Israel.
Anashauri nchi za Afrika zifunge ubalozi wa Israel, zisitishe uhusiano wa kidiplomasia na wa kibiashara.
“Kufunga ubalozi ni hatua ya chini kabisa. Hatuwezi kuruhusu wauaji wa halaiki kuwa miongoni mwetu,” asema Jo. “Kwa nini watu kama hawa wawe na balozi Afrika?”