
Winga wa Namungo FC, Herbert Lukindo ameukubali muziki wa Ligi Kuu Bara na kutoa tahadhari kwa timu yake kusahihisha mapema makosa yaliyotokea kwenye michezo mitatu ya mwanzo ili kuhakikisha inafanya vizuri.
Katika msimu huu, Namungo imeshacheza mechi tatu za Ligi Kuu Bara dhidi ya Pamba Jiji, Tanzania Prisons na Simba ambapo imevuna alama nne baada ya kuifunga Tanzania Prisons bao 1-0, sare ya 1-1 na Pamba Jiji na kupoteza kwa mabao 3-0 dhidi ya Simba.
Timu hiyo ya mkoani Lindi inakamata nafasi ya tisa kwenye ligi baada ya kuvuna pointi nne katika mechi tatu, ikishinda moja, sare moja na kupoteza moja, huku ikifunga mabao mawili na kuruhusu manne.
Akizungumza na Mwanaspoti, Lukindo aliyejiunga na Namungo msimu huu kwa mkataba wa mwaka mmoja akitokea Ken Gold ya Mbeya, alisema kila timu waliyokutana nayo imejiandaa vizuri na hakuna mnyonge, hivyo inapaswa kuwa imara zaidi ili kuvuna alama kwa wapinzani wake.
“Ligi ni ngumu, kila timu imejiandaa vizuri. Kwa hiyo nina kazi ya ziada ya kufanya ili kuisaidia timu yangu. Malengo ni kuhakikisha timu inakaa sehemu salama, ndipo malengo binafsi yatatimia endapo timu itakuwa inafanya vizuri,” alisema Lukindo.
Nyota huyo wa zamani wa Mbao na Biashara United alisema kikosi chao kitarudi kikiwa imara zaidi baada ya mapumziko kupisha mechi za timu za taifa kwani watafanyia kazi baadhi ya udhaifu ulioonekana katika mechi za mwanzo ikiwemo kuruhusu mabao 3-0 mbele ya Simba.
“Kikosi chetu kiko sawa, naamini tutaendelea kukaa sawa kwenye kipindi hiki cha mapumziko.. tutaendeleza mazuri yetu na kufanyia kazi upungufu wetu,” alisisitiza winga huyo.