Dar es Salaam. Ni wazi kuwa baadhi ya mashabiki wa msanii wa muziki wa singeli DJ Mushizo wamepata faraja baada ya mkali huyo kurudi uraiani baada ya kulazwa hospitalini kwa zaidi ya mwezi. Ikiwa ni tangu alipopata ajali ya moto Juni 12, 2025 wakati akiwa nyumbani kwake Tabata jijini Dar es Salaam.
Mushizo ambaye alilazwa katika Hospitali ya Amana, ameliambia Mwananchi licha ya kupata ajali hiyo, kuna mambo mengi ya baraka yamefunguka kwake.
“Ajali ile imetokea kwa mapenzi ya Mungu, lakini pia baraka zimekuwa nyingi. Hakuna mabadiliko mabaya kila kitu kipo sawa. Hii ajali kwangu mimi haijanirudisha nyuma naona kama imenipa nguvu ya kuendelea mbele zaidi.
Mushizo anasema kwa sasa maendeleo yake ni mazuri tofauti na ilivyokuwa awali.
“Mimi niko sawa Mungu mwema nina makovu tu madogo madogo ndiyo naendelea nayo na dawa ndogondogo. Lakini nadhani mashabiki wangu watoe hofu kwani wanaona hata ninavyopromoti kazi zangu kwenye mitandao,” anasema.
Hata hivyo Mushizo hajarudi mikono mitupu kwa mashabiki wake, kwani ameachia wimbo wake kwanza tangu atoke hospitali uitwao ‘Staki Mazoea’ akiwashirikisha Dogo Mallo, Kusah na Country Wizzy.
“Project ilikuwapo lakini ilikuwa bado haijatimia kwa hiyo nilivyopona nikakamilisha baadhi ya verse, mastering na video. Mwanzo niliowashirikisha hawakuwepo kwenye wimbo lakini nilivyopata nafuu niliwatumia tukamaliza jambo,”anasema
Mushizo anasema kabla ya kumshirikisha msanii yeyote kwenye kazi yake huzingatia kipaji na uwezo wake.
“Hakukuwa na ugumu katika mlolongo wangu wa kufanya kazi na Kusah na Country Wizzy. Ni kawaida kutokana na jinsi ninavyofanya kazi zangu. Na wao wanajua tukifanya kazi pamoja inafika sehemu fulani,” anasema.
Licha ya hayo Mushizo anajitofautisha na wasanii wengine wa Singeli kama D Voice ambaye amewahi kufanya aina mbalimbali za muziki nje ya singeli. Lakini kwa Mushizo anasema hawezi kuvuka nje ya singeli.
“Siwezi kufanya muziki nje na singeli labda nichukue aina nyingine za muziki nilete katika singeli kama ambavyo nimefanya kwenye kazi yangu ‘Sitaki Mazoea’. Siwezi kuchanganya watu wamenizoea huku na ndiko kumenitambulisha
“Muziki wa Singeli umekuwa mkubwa, unaona hata ngoma yangu ina siku chache lakini tayari inaongoza. Inashindana na nyimbo za Bongo Fleva. Zamani haikuwa rahisi kuwa hivyo zamani licha ya kuwa nimetoka kwenye changamoto lakini matokeo yamekuwa makubwa,”anasema
Hata hivyo mwonekano wa Mushizo wa sasa umekuwa ukiibua maswali kutoka kwa baadhi ya mashabiki wake haswa kwenye mitandao ya kijamii wakidai amenenepa sana. Hilo nalo msanii huyo amelijipu kupitia Mwananchi
“Ni kitu kizuri, imeonesha jinsi gani sijawa na changamoto na hata nilivyokuwa na changamoto nilikuwa na watu wengi ambao wananitia moyo, kuhakikisha nakuwa sawa. Watu wengine wakitoka hospitali wanakuwa wamedhohofika, wamekonda.
“Hadi kuwa sawa huwa inachukua muda. Lakini kwangu mimi ndugu zangu wamekuwa pamoja na mimi na kunipa moyo hivyo ni vitu ambavyo vilikuwa vinanitia nguvu,”anasema
Utakumbuka msanii huyo alipopata ajali Meneja wake Msaidizi, Ally Masupu alisema chanzo cha moto huo uliomdhuri Mushizo ni shoti ya umeme.
“Chanzo cha moto ni shoti ya umeme pale ndani anapoishi Tabata. Yeye alikuwa amelala hana habari, alipokuja kushtuka akakuta moto umeshashika kasi, hakuweza kujiokoa mwenyewe,” alisema Masupu.