
Nahodha wa Manchester United, Bruno Fernandes amesema kuwa fursa ya kucheza Kombe la Dunia 2026 sio sababu pekee iliyofanya akatae kujiunga na Al Hilal ya Saudi Arabia katika dirisha lililopita la usajili la majira ya kiangazi.
Mchezaji huyo amesema kuwa mapenzi aliyonayo kwa Man United ndio yamechangia kwa kiasi kikubwa kukataa ofa nono ya Al Hilal ambayo ilionekana kuweka nguvu nyingi kuhakikisha inamsajili katika dirisha la usajili lililopita.
Timu hiyo ya Saudi Arabia ilitenga dau la Pauni 100 milioni (Sh326 bilioni) kwa ajili ya kuishawisha Man United iwauzie Fernandes huku mchezaji huyo akiwekewa mezani mkataba ambao ulikuwa na thamani ya Pauni 200 milioni (Sh651 bilioni).
Hata hivyo pamoja na Manchester United kuwa na mwenendo usioridhisha katika msimu uliopita, mchezaji huyo raia wa Ureno aliamua kubakia huku ikidaiwa kwamba alihofia kwenda Saudi Arabia kwa ajili ya kulinda nafasi yake katika fainali zijazo za kombe la Dunia.
Fernandes amesema kuwa taarifa zinazotolewa kuwa Kombe la Dunia ndio limesababisha akatae ofa ya Saudi Arabia ni takataka.
“Sikufunga mlango wa kwenda Saudi Arabia kwa sababu ya Kombe la Dunia. Hilo halikuwa akilini mwangu. Nilitaka kubakia Manchester United na klabu ilitaka nibakie. hiyo ndivyo ilivyokuwa.
“Nina furaha mahali nilipo. Vinginevyo nisingeweza kubakia. Lakini hiyo hainiathiri,” amesema Fernandes.
Licha ya Manchester United kutofanya vizuri katika miaka ya hivi karibuni, Fernandes ameonyesha kiwango bora ambacho kimekuwa kikizivutia klabu nyingi.
Tangu alipoanza kuitumikia Man United mwaka 2020, mchezaji huyo amecheza idadi ya mechi 298, akifunga mabao 100 na kupiga pasi za mwisho 86.