#HABARI: Wakulima na wakazi wa Kijiji cha Kasanda wilayani Kakonko mkoani Kigoma, wamesema ujenzi wa ghala la kuhifadhia chakula katika kijiji hicho utawanufaisha kwa kiasi kikubwa na kuwasaidia kuongeza thamani ya mazao hivyo kukuza uchumi wao na taifa kwa ujumla.
Hayo yamejiri kwenye hafla fupi ya makabidhiano ya ghala la kuhifadhia chakula iliyofanyika katika Kijiji cha Kasanda wilayani Kakonko mkoani Kigoma ambapo baadhi ya wananchi wakazi wa Kijiji cha Kasanda wameeleza namna watakavyonufaika na ghala hilo baada ya kuteseka kwa muda mrefu kwa kukosa namna ya kuhifadhi mazao hayo.
Kwa upande wake Mkuu wa Ofisi ya Shirika la Chakula Duniani Kigoma,Saidi Johari, ameeleza kuwa wafadhili wengi wanahitaji kuona matokeo chanya ya fedha kwa ubora wa matumizi ya miradi husika na kwamba ghala hilo ni mkombozi kwa wakulima.
Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Evance Malasa, baada ya makabidhiano ya ghala hilo anasema kuwa ni vema wananchi kutunza mali na miradi mbali mbali wanayokabidhiwa ili viweze kuwasaidia katika kujiletea maendeleo.