Dar es Salaam. Ni muda sasa Nandy na Zuchu wamekuwa wakijitahidi kufanya kazi bora zaidi ili kudhihirisha uwezo wao kimuziki, jambo lililoleta ubunifu na motisha kwa wasanii wengine wa kike ndani ya Bongofleva.

Ingawa mashabiki mara nyingi wamekuwa wakiwalinganisha, wote ni wasanii wenye vipaji vikubwa, sauti nzuri na uwezo wa kutoa nyimbo zinazowakosha mashabiki, lakini kimuziki wanazidiana kete, twende pamoja:

1. Tayari Nandy ametoa Extended Playlist (EP) tatu, Taste (2021), Wanibariki (2021) na Maturity (2022), pamoja na albamu moja, The African Princess (2018) yenye nyimbo 13 na urefu wa dakika 44. Wakati Zuchu ana EP moja, I Am Zuchu (2020) ambayo ndio ilimtambulisha, huku akiwa na albamu moja pia, Peace and Money (2024) ikiwa na nyimbo 13 na urefu wa dakika 43.

2. Zuchu ameshinda tuzo mbili kutoka African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA) zinatolewa Marekani. Ameshinda kama Msanii Bora Chipukizi 2020, na Msanii Bora wa Kike Afrika Mashariki 2022. Kwa upande wake Nandy, ameshinda AFRIMMA mara moja  Kama Msanii Bora wa Kike Afrika Mashariki 2021, hivyo msimu uliofuatia ndipo Zuchu akanyakua kipengele hicho.

3. Nandy ni mkali wa melodi, wakati Zuchu anatisha zaidi kiuandishi na ndio sababu nyimbo zake nyingi ameandika mwenyewe, ila Nandy kuna baadhi kaandikiwa na wasanii wenzake.

4. Nyimbo alizoandikiwa Nandy ni Kivuruge, Njiwa, Hallelujah na Do Me (Jay Melody), Bugana, New Couple na Dah! (Billnass), Wasikundanganye (Marioo), Nibakishie (Kusah) na Napona (Lody Music).

5. Tangu Aprili 2020 hadi sasa, video za Zuchu katika mtandao wa YouTube zimetazamwa zaidi ya mara milioni 960.2, huku za Nandy tangu Julai 2016 hadi sasa, zikitazamwa zaidi ya mara milioni 297.5.

6. G Nako, Jux, Darassa na Joeboy kutokea Nigeria, ndio wanamuziki pekee waliofanikiwa kufanya kolabo na Nandy (Dah! Remix, Sweety, Loyalty na Number One), na Zuchu (Hapo, Nidhibiti, Romeo na Nobody) kwa pamoja.

7. Zuchu ndiye mwanamuziki wa kwanza wa kike Afrika Mashariki kufikisha wafuatiliaji (subscribers) milioni 1 YouTube, kisha wakafuatia Nandy na Rose Muhando, staa wa muziki wa Injili.

8. Kwa Tanzania, mtiririko wa kufikisha wafuatiliaji milioni 1 YouTube upo hivi Diamond, Harmonize, Rayvanny, Mbosso, Zuchu, Alikiba, Lava Lava, Nandy, Marioo, Aslay, Rose Muhando, Jux na Jay Melody.

9. Zuchu ameshinda tuzo saba za muziki Tanzania (TMA) baada ya kushiriki kwa misimu miwili pekee (2022 & 2023, huku Nandy akishinda nne katika misimu mitatu (2021, 2022 & 2023).

10. Nandy ameendelea kujisimamia mwenyewe kimuziki kupitia lebo yake, The African Princess Label ambayo ilimtoa Yammi kimuziki kupitia EP yake Three Hearts (2023) yenye nyimbo tatu.

Lakini Zuchu anasimamiwa na WCB Wasafi, lebo yake Diamond Platnumz ambayo ndani ya miaka 10 imefanikiwa kuwasimamia wasanii wanane huku wa kike wakiwa wawili tu – mwingine ni Queen Darleen.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *