
Wimbi la watu maarufu nchini kuuza vipodozi limekuja kwa kasi mno, kiasi kwamba linashawishi jamii kuhadaika kwenye matumizi ya vipodozi kila wavionapo vinatangazwa na mtu maarufu kwa angalizo la kung’aa kistaa au ‘kuglow’ kama wanavyoita, ngozi kuwa laini ya kuteleza na inayovutia bila kuzingatia athari za ngozi kwa mtumiaji vipodozi atakavyotumia.
Jana, kwenye Gazeti la Mwananchi tulichapisha habari kuhusu ‘wanawake wanavyonaswa mtego wa uraibu wa vipodozi’, hii ni kuonyesha jinsi gani wanawake wanavyoingia katika mtego huu wa matumizi ya vipodozi pasipo kuhusisha ushauri wa daktari, wao wakizingatia zaidi matokeo ya nje ya ngozi bila kujua hatari anayojitengenezea ya matumizi holela ya vipodozi kwa kuangalia msanii fulani ana ngozi nzuri kwa hiyo atakuwa anatumia kipodozi hicho.
Video na picha za watu maarufu na wenye ushawishi kwenye mitandao ya kijamii nchini zimegeuka mwalimu mpya wa urembo kwa jamii.
Hata hivyo, nyuma ya urembo huu, kuna gharama kubwa za kifedha, muda, na hata athari za kiafya na kisaikolojia zinazojitokeza kwa baadhi ya watumiaji.
Matumizi ya vipodozi holela huleta madhara makubwa kwa ngozi, mara nyingi madhara yake huonekana baada ya mtumiaji kuchanganya vipodozi tofauti kwenye ngozi, ambavyo huua seli za nje ya ngozi hivyo mtumiaji kuanza kubabuka ngozi au kutoka magamba, wengine kubadilika rangi na kuwa nyekundu, mara nyingi hupata maumivu sana wakati wa jua kali.
Mraibu wa vipodozi anapoacha kutumia vipodozi hivyo mara nyingi ngozi yake huanza kuharibika kwa hiyo itamlazimu kuendelea kutumia, na hapo ndipo hatari inapokuja.
Kwa upande wa shuhuda mmoja aliyewahi kutumia alisema aliingia kwenye mtego wa matangazo yanayodai kuwa bidhaa fulani zinatibu haraka chunusi na makovu. Alijikuta akitumia zaidi ya Sh600,000 ndani ya miezi mitatu bila mafanikio, baada ya kuona video za ‘influencers’ wakizisifia. Lakini badala ya kusaidia tatizo, zilimletea madoa na vipele kwenye ngozi yake.
Changamoto ya bidhaa nyingi za vipodozi ni kuwa na kemikali hatari kwa ngozi na wengi hutumia bila kujua kilichomo ndani yake na madhara yanayoweza kutokea.
Jamii ichukue tahadhari kwenye matumizi haya maana wengi hununua bidhaa bila kujua viambato vilivyomo. Baadhi ya vipodozi vina kemikali hatari kama hydroquinone na mercury, ambazo zinaweza kuharibu ngozi au hata kuathiri viungo vya ndani ya ngozi.
Matumizi hayo ya vipodozi holela mtumiaji anaweza kupata madoa, michirizi na chunusi za kudumu, haya ni matokeo ya kutumia bidhaa isiyoendana na ngozi.
Tunashauri matumizi sahihi ya vipodozi yaendane na bidhaa bora ambayo inaendana na ngozi yako, au ukiona kuna utofauti basi fuata ushauri wa daktari kipi upake kutokana na aina ya ngozi yako na si kukurupuka kutumia bidhaa tu za mtandaoni kisa msanii maarufu anapaka.
Usipake kitu bila kujua aina ya ngozi yako.
Kutunza ngozi ni jambo muhimu kwa afya na mwonekano wa mtu, lakini ni muhimu kufanya hivyo kwa njia salama, yenye uelewa na isiyoathiri afya wala uchumi wako. Tunza ngozi yako kwa kutumia vitu vilivyothibitishwa na daktari, vitu visivyokuwa na kemikali hatarishi kwenye ngozi yako.
Epuka kutumia bidhaa nyingi kwa wakati mmoja bila kuelewa kazi yake, kununua bidhaa kwa sababu tu zimependekezwa na watu maarufu, kunaweza kukuingiza kwenye matatizo. Kulinda ngozi yako ni wajibu wako mwenyewe.