Dar es Salaam. Kifo cha Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Shinyanga, Asha Mwetindwa, kimesababisha kesi ya uhaini inayomkabili Tundu Lissu kuahirishwa kabla ya muda wa mahakama kumalizika.

Kesi hiyo, inayosikilizwa katika Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam, iliendelea leo, Oktoba 15, 2025, kwa mshtakiwa Lissu, ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kuendelea kumhoji kwa maswali ya dodoso shahidi wa pili wa Jamhuri.

Shahidi huyo ni Mkaguzi wa Polisi, John Kaaya, kutoka Kitengo cha Upelelezi wa Makosa ya Mtandaoni, Dawati la Doria Mtandaoni, Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Makao Makuu, Dar es Salaam.

Hata hivyo, kutokana na taarifa za msiba, kesi hiyo iliahirishwa saa 5:00 asubuhi, badala ya saa 10:00 au 11:00 jioni.

Katika kesi hiyo, Lissu anakabiliwa na shtaka la uhaini akidaiwa kutoa maneno ya kuitishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kinyume cha kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.

Anadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania mwenye utii kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alitoa maneno ya kuitishia Serikali na kuonesha nia hiyo kwa kuchapisha maneno hayo katika mitandao ya kijamii kuwa:

“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kukinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”

Kesi hiyo, inayosikilizwa katika Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam, iko mbele ya jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Iringa, Dunstan Ndunguru. Majaji wengine ni James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.

Leo, Oktoba 15, kabla ya Lissu kuanza kumhoji shahidi huyo, kiongozi wa jopo la waendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Lenatus Mkude, aliieleza mahakama kuhusu msiba huo na kuomba ruhusa ya kuhudhuria maziko.

Mkude aliieleza mahakama kuwa, kutokana na madhehebu ya marehemu ambaye ni Muislamu, mwili utazikwa leo saa saba mchana, hivyo akaomba kesi iendelee kwa muda mfupi kabla ya kuahirishwa ili kutoa nafasi kwao kuhudhuria maziko.

“…Juzi, baada ya kuahirisha shauri hili, tulipokea taarifa ya msiba wa mtumishi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Shinyanga. Kwa mujibu wa taratibu, tumekuwa tukishirikiana katika matukio kama haya. Kwa kuwa ni haki ya mshtakiwa kesi iendelee, tunaomba mahojiano yaendelee hadi saa tano kabla ya kuahirisha,” aliomba Mkude.

Lissu amesema hana pingamizi na maombi hayo, lakini akawataka mawakili wa Serikali wamfikishie salamu zake za pole kwa wafiwa.

Baada ya taarifa hiyo, Lissu alianza kumhoji shahidi maswali ya dodoso kuhusu ushahidi alioutoa mahakamani. Ilipofika saa 5:00 asubuhi, kesi ikaahirishwa kama Jamhuri ilivyoomba.

Jaji Ndunguru ameahirisha kesi hiyo hadi kesho, Oktoba 16, ambapo mshtakiwa ataendelea na mahojiano na shahidi huyo.

Sehemu ya mahojiano kati ya mshtakiwa Lissu na shahidi ilikuwa kama ifuatavyo:

Lissu: Baada ya yote niliyokuuliza siku ya Jumatatu, ulipata muda wa kuangalia tena ile video ya Aprili 3, 2025, ambayo wewe unasema uliiona Aprili 4, 2025?

Shahidi: Hapana.

Lissu: Naomba uieleze mahakama kama unajua video hiyo ilipelekwa kwenye mitandao ya Arusha One Digital, Mwanzo TV, Chanzo TV na Jambo TV.

Shahidi: Sifahamu.

Lissu: Waeleze waheshimiwa majaji kama unafahamu kwamba kusambaza au kusaidia kusambaza maandiko au taarifa zinazohusu uhaini, nalo ni kosa la uhaini.

Shahidi: Sifahamu.

Lissu: Naomba uwaeleze waheshimiwa majaji kama unafahamu kwamba kutoa kauli tu haliwezi kuwa kosa la uhaini kwa mujibu wa sheria zetu.

Shahidi: Sifahamu.

Lissu: Ni kweli au si kweli kwamba ili kosa liwe la uhaini, kwanza lazima kuwe na nia ya kutenda huo uhaini?

Shahidi: Kweli.

Lissu: Na ni kweli kwamba hiyo nia lazima ithibitishwe ama kwa maandishi au kwa matendo?

Shahidi: Ni kweli.

Lissu: Ni kweli au si kweli kwamba video ya Aprili 3 ilichapishwa kwenye mitandao kama Jambo TV na mingineyo?

Shahidi: Aliyechapisha sifahamu.

Lissu: Ni kweli au si kweli kwamba mkutano wangu wa Aprili 3 ulirushwa mubashara na Jambo TV?

Shahidi: Kweli.

Lissu: Na ni kweli kwamba mimi (Lissu) si mfanyakazi wa Jambo TV na sina uhusiano wowote na Jambo TV?

Shahidi: Sikufanya upelelezi wa wahusika wa Jambo TV.

Lissu: Uliulizwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Job Mrema, kama unaweza kuitambua ile video na maudhui yake, ukasema unaweza kuitambua na ukasema mimi (Tundu Lissu) nimevaa kombati na nyuma kulikuwa na bendera.

Shahidi: Ndiyo.

Lissu: Sasa hayo maneno uliyaandika kwenye maelezo yako ya polisi siku tatu baada ya kuiona hiyo video?…

Shahidi: Sikuandika.

Lissu: Umezungumza sana juu ya hiyo video, ukawaonesha wakubwa zako, ukamuonesha SSP George Bagyemu, ukaipakua, sasa naomba uwaeleze majaji kama hiyo flash uliiwasilisha mahakamani.

Shahidi: Bado sijaiwasilisha.

Lissu: Kwa hiyo ni sahihi nikisema hakuna mtu aliyeiona isipokuwa wewe. Majaji hawajaiona wala mawakili wa Serikali hawajaiona?

Shahidi: Kweli.

Lissu: Waeleze waheshimiwa majaji, kwa ufahamu wako wa Katiba, kama kuna utaratibu umeandikwa wa namna ya kuzuia uchaguzi.

Shahidi: Upo.

Lissu: Sasa ni kweli kwamba uchaguzi mkuu unaendeshwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi?

Shahidi: Kweli.

Lissu: Na ni kweli kwamba tume hiyo ni chombo huru kisichotakiwa kuingiliwa na mamlaka yoyote?

Shahidi: Sikumbuki.

Lissu: Waeleze waheshimiwa majaji kama Serikali ya nchi hii inaendesha uchaguzi mkuu.

Shahidi: Kweli.

Lissu: Na mimi mashtaka yanayonikabili yanasema nilitaka kuhamasisha watu wazuie uchaguzi mkuu wa 2025. Ni kweli au si kweli?

Shahidi: Inategemea.

Lissu: Umeiangalia vizuri hiyo hati ya mashtaka?

Shahidi: Sijaiangalia.

Lissu: Kwa hiyo hujui nashtakiwa kwa nini?

Shahidi: (Kimya).

Lissu: Kwenye hayo maneno niliyoyasema, hakuna neno hata moja nimetaja Serikali. Ni kweli au si kweli?

Shahidi: Serikali ipo.

Lissu: Shahidi, kwenye visomo vyako ulisoma sheria za jinai?

Shahidi: Kweli.

Lissu: Na umesoma pia sheria yetu kuu ya jinai?

Shahidi: Nimesoma.

Lissu: Mimi nimeshtakiwa kwa kosa la uhaini chini ya kifungu cha 39(2)(d). Sasa waeleze waheshimiwa majaji kama katika kifungu hicho neno “kutishia” limefafanuliwa.

Shahidi: Sikumbuki.

Lissu: Nikikuambia kwamba hilo neno “kutishia” halijafafanuliwa mahali popote kwenye Penal Code, utasemaje?

Shahidi: Sifahamu.

Lissu: Maneno “majaji ni wa CCM” niliyoyazungumza, je, hayo ni ya kihaini?

Shahidi: Hakuna sehemu wanasema ni ya kihaini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *