Morocco imetwaa ubingwa wa Kombe la Dunia la Vijana chini ya umri wa miaka 20 baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mabingwa watetezi Argentina jijini Santiago Chile.
Mabao mawili ya Mohamed Zabiri katika kipindi cha kwanza, yametosha kuipa timu ya taifa ya Morocco chini ya umri wa miaka 20 taji hilo ambalo ni la kwanza la dunia kwenda kwa taifa la Morocco.
Zabiri alifunga bao la kwanza katika dakika ya 12 na la pili akapachika katika dakika ya 29 na kuifanya timu yake iingie katika historia ya kuwa timu ya pili ya Afrika kuwahi kutwaa taji hilo baada ya Ghana iliyofanya hivyo mwaka 2009.
Morocco pia imekuwa timu ya kwanza baada ya miaka 42, kuifunga Argentina katika mechi ya fainali ya Kombe la Dunia chini ya umri wa miaka 20.
Mara ya mwisho kwa Argentina kupoteza mechi ya fainali ya mashindano hayo ilikuwa ni 1983 ilipopoteza mbele ya Brazil wakatin fainali hizo zilipofanyika Mexico.
Ni safari ambayo haijawa nyepesi kwa Morocco hadi ikafika katika hatua hiyo ya fainali ambayo imeondoka na taji la mashindano hayo.
Timu hiyo kabla ya kuichapa Argentina, imekutana na timu nyingi ngumu lakini iliweza kuruka vihunzi hivyo na kulifikia taji.
Katika hatua ya makundi iliibuka na ushindi dhidi ya Brazil na Hispania na katika hatua ya 16 bora ikaichapa Korea Kusini.
Kwenye robo fainali ikaifunga Marekani na ikapata ushindi dhidi ya Ufaransa katika hatua ya nusu fainali.
Mchezaji Bora wa mashindano hayo ametangazwa kuwa Othmane Maamma wa Morocco huku Mfungaji Bora akiwa ni Benjamin Cremaschi wa Marekani na Kipa Bora ni Santino Barbi wa Argentina.