
Rais wa mpito wa Madagascar Kanali Michael Randrianirina amemteua mfanyabiashara Herintsalama Rajaonarivelo kuwa waziri mkuu mpya wa nchi hiyo na kumuapisha katika hafla rasmi iliyofanyika kwenye Ikulu ya Jimbo la Iavoloha.
Randrianirina amesema uteuzi wa Rajaonarivelo ulifanywa kufuatia pendekezo la wajumbe wa Bunge la Taifa.
“Amechaguliwa kwa ujuzi wake, uzoefu, na uhusiano na mashirika ya kimataifa,” ameeleza kanali huyo wa jeshi.
Rajaonarivelo amechukua nafasi ya Zafisambo Ruphin Fortunat, aliyeteuliwa na Rais wa zamani Andry Rajoelina kuwa waziri mkuu wa Madagascar Oktoba 6, kufuatia kuvunjwa kwa serikali mnamo Septemba 29.
Rajaonarivelo, asiyejulikana sana katika ulingo wa kisiasa, alishikilia nyadhifa kadhaa za juu katika sekta ya binafsi, ikiwa ni pamoja na kuwa mwenyekiti wa zamani wa bodi ya wakurugenzi ya Benki ya BNI Madagascar.
Akiwa na shahada ya uzamili katika uchumi wa viwanda na uchumi wa biashara, Rajaonarivelo alikuwa mshauri wa kimataifa wa mashirika kadhaa ya kimataifa kama vile Benki ya Dunia, EU, Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika, Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika, na Tume ya Bahari ya Hindi.
Rais Randrianirina aliapishwa kuwa rais siku ya Ijumaa iliyopita kufuatia siku kadhaa za maandamano dhidi ya serikali ya Rais aliyeondolewa madarakani Rajoelina.
Maandamano yaliyoongozwa na vijana yalizuka Septemba 25 kutokana na uhaba mkubwa wa maji na umeme, pamoja na madai ya rushwa, baadaye yaligeuka haraka kuwa wito wa kumtaka aliyekuwa rais wa nchi hiyo Rajoelina ajiuzulu…/