Bilbao, Hispania. Klabu ya Athletic imetoka nyuma na kuichapa Qarabag mabao 3-1 na kupata ushindi wake wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu, baada ya kiungo wa Qarabag, Leandro Andrade, kuweka historia kwenye soka la Ulaya leo Oktoba 22, 2025, kwenye Dimba la San Mamés, Hispania.

Andrade aliwapatia Qarabag uongozi baada ya sekunde 48 tu, akitumia makosa ya ulinzi kati ya Aymeric Laporte na Aitor Paredes na kumtungua kipa Unai Simón.

Kwa kufanya hivyo, mchezaji huyo kutoka Cape Verde alikuwa wa kwanza katika historia ya mashindano makubwa ya soka barani Ulaya kufunga bao katika dakika ya kwanza ya mechi tatu tofauti.

Athletic Club iliongeza kasi na hatimaye ikasawazisha dakika ya 40 kupitia Gorka Guruzeta aliyemalizia vyema akiwa ana kwa ana na kipa.

Baada ya mapumziko, timu ya Bilbao iliendelea kutawala na kupata bao la pili kupitia mchezaji wa akiba Robert Navarro, aliyepiga shuti la kupinda hadi kwenye kona ya juu dakika tano baada ya kumrithi Nico Williams.

Muda mfupi baada ya Yuri Berchiche kuokoa, mpira wa Oleksii Kashchuk uliokuwa unaelekea kufunga bao la kusawazisha, Guruzeta alifunga bao lake la tatu katika mechi tatu za Ligi ya Mabingwa kwa kombora kali lililoenda chini.

Huu ulikuwa ni ushindi wa pili pekee katika mechi 10 zilizopita kwa kikosi cha Ernesto Valverde, ambacho kilianza kampeni ya Ulaya kwa kupoteza 2-0 dhidi ya Arsenal na 4-1 dhidi ya Borussia Dortmund.

Katika mechi ya nne ya hatua ya makundi, Athletic Club itasafiri kuvaana na Newcastle kwenye Uwanja wa St James’ Park (Novemba 5, 2025), huku Qarabag ikiipokea Chelsea mjini Baku siku hiyohiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *