Hii ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya shirika hilo iliyotolewa leo Jumatatu, tarehe 27 mwezi Oktoba 2025, ikipewa jina “Katika Hatari na Ukosefu wa Ufadhili wa Kutosha,” inayotokana na utafiti wa kimataifa ulioshirikisha mashirika 428 ya haki za wanawake na asasi za kiraia.

Ripoti hiyo imeonesha kuwa, kutokana na kupunguzwa kwa ufadhili kutoka kwa serikali mbalimbali, idadi ya wanawake wanaokumbwa na ukatili imeongezeka, huku huduma muhimu zinazowasaidia wanawake na wasichana zikiendelea kudhoofika na sauti za utetezi zikinyamazishwa, hali inayoweza kuathiri mamilioni ya wanawake na wasichana duniani.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo:

  • Asilimia 34 ya mashirika yamesitisha au kufunga kabisa programu za kukomesha ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.
  • Zaidi ya asilimia 40 yamelazimika kupunguza au kusitisha huduma za kuokoa maisha kama vile hifadhi salama, msaada wa kisheria, usaidizi wa kisaikolojia na huduma za afya kutokana na upungufu wa ufadhili.
  • Asilimia 78 ya mashirika yameripoti kupungua kwa upatikanaji wa huduma muhimu kwa waathirika, huku asilimia 59 yakibainisha ongezeko la hali ya ukosefu wa adhabu na kuridhika kwa jamii na matukio ya ukatili.
  • Takribani asilimia 25 ya mashirika yamesema kwamba yamelazimika kusimamisha au kusitisha kabisa miradi ya kuzuia ukatili kabla haujatokea.
Nafasi salama kwa wanawake katika kambi ya wakimbizi wa ndani huko Bentiu, Sunda Kusini

© UNOCHA/Alioune NDIAYE

Nafasi salama kwa wanawake katika kambi ya wakimbizi wa ndani huko Bentiu, Sunda Kusini

Wito wa haraka kwa serikali na wafadhili

Kalliopi Mingeirou, Mkuu wa Kitengo cha Kukomesha Ukatili Dhidi ya Wanawake na Wasichana, cha UN Women, amesema:

“Mashirika ya haki za wanawake ndio uti wa mgongo wa maendeleo ya kupinga ukatili wa kijinsia, lakini sasa yanasukumwa ukingoni mwa kusitisha shughulizake. Hatuwezi kuruhusu kupunguzwa kwa ufadhili kufuta mafanikio ya miongo kadhaa yaliyopatikana kwa taabu.”

Ameongeza kuwa “Tunatoa wito kwa serikali na wafadhili kulinda, kuongeza na kufanya ufadhili kuwa rahisi na wa muda mrefu zaidi. Bila uwekezaji endelevu, ukatili dhidi ya wanawake na wasichana utaendelea kuongezeka,”

Ukatili dhidi ya wanawake unasalia kuwa changamoto kubwa

Kwa mujibu wa ripoti hiyo Ukatili dhidi ya wanawake na wasichana unabaki kuwa moja ya ukiukaji mkubwa zaidi wa haki za binadamu duniani.

Inakadiriwa kuwa wanawake milioni 73 sawa na takriban mwanamke mmoja kati ya watatu duniani wamewahi kukumbwa na ukatili wa kimwili au kingono, mara nyingi kutoka kwa wenza wao wa karibu.

Mapema mwaka huu, UN Women imeonya kuwa mashirika mengi yanayoongozwa na wanawake katika maeneo yenye migogoro yalikuwa yakikabiliwa na ukata mkubwa, na takriban nusu yake yakiwa katika hatari ya kufungwa onyo ambalo sasa limethibitishwa na matokeo ya ripoti hii mpya. 

Hofu ya kudorora kwa sheria na ulinzi kwa wanawake

Matokeo ya ripoti pia yameonesha:

  • Asilimia 5 tu ya mashirika hayo yanatarajia kuweza kuendeleza shughuli zao kwa miaka miwili au zaidi.
  • Asilimia 85 yanatabiri kudorora kwa kasi kwa sheria na ulinzi kwa wanawake na wasichana.
  • Na asilimia 57 yanaripoti wasiwasi mkubwa juu ya kuongezeka kwa hatari kwa watetezi wa haki za binadamu wa kike.

Upungufu huu wa ufadhili unajitokeza sambamba na kuongezeka kwa pingamizi dhidi ya haki za wanawake katika nchi moja kati ya nne, hali inayolazimisha mashirika mengi kuelekeza nguvu zao kwenye huduma za msingi badala ya utetezi wa muda mrefu unaosababisha mabadiliko ya kweli.

Ripoti, sambamba na miaka 30 ya Azimio la Beijing

Ripoti jiyo “Katika Hatari na Ukosefu wa Ufadhili wa Kutosha” imetolewa wakati ambapo dunia inaadhimisha miaka 30 tangu kupitishwa kwa Azimio la Beijing na Jukwaa la Utekelezaji, mwongozo wa maendeleo uliopitishwa na serikali mbalimbali kwa lengo la kufanikisha usawa wa kijinsia na haki za wanawake, huku kukomesha ukatili dhidi ya wanawake kikiwa kipengele kikuu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *