
“Bila shaka, yaliyotokea Geneina hayako kwenye video vizuri kama ilivyokuwa Al Fasher. Video za RSF wenyewe Geneina hazikuwa na muonekano mzuri kama ilivyo Al Fasher,” Ishaq amesema.
Waziri huyo amesisitiza kuwa video za uhalifu wa RSF zimekuwa “sehemu ya waasi hao kutumia kama silaha kupata ushindi dhidi ya upande mwingine.”
“Furaha ya kuua yenyewe inawapa hisia za ushindi. Kisaikolojia, ni ugonjwa wa aina fulani wa kupata ushindi. Ni kama kumkabili mpinzani wako kwa mafanikio, na hali hii imekuwa sehemu muhimu ya silaha kwa RSF,” aliongeza.
“Kama RSF imebaki Al Fasher, watamuangamiza kila binadamu Darfur. Haya ni mauaji ya kikabila, na kila mtu anahusika kwa kukaa kimya,” waziri huyo alionya.
Alisisitiza kuwa kukaa kimya kwa jamii ya kimataifa kutawapa nguvu RSF kuendeleza uhalifu huko Al Fasher na nchini kote.
Mashirika ya misaada Al Fasher, Ishaq anasema misaada iliyofikishwa Tawila kupitia mashirika mengine haitoshi kukidhi mahitaji ya maelfu ya familia zilizokimbia makazi yao katika mji huo.
Alieleza kuwa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yanashindwa kuingia eneo hilo, kwa kuwa ni hatari kwa maisha ya raia na wafanyakazi wengine wa misaada.
“Lakini tunawasiliana na wadau wote na kujaribu kusaidia kupeleka fedha bila kutangaza ,” alisema.
Oktoba 26, RSF ilidhibiti Al Fasher na kutekeleza “mauaji ya kikatili” dhidi ya raia, kulingana na mashirika ya eneo hilo na kimataifa, huku kukiwa na onyo kuwa mauaji hayo yanawexa kuleta mgawanyiko mkubwa nchini Sudan.
Siku ya Jumatano, kiongozi wa RSF Mohamed Hamdan Dagalo (Hemetti) alikiri kuwa kulikuwa na “ukiukwaji” kutoka kwa wapiganaji wake Al Fasher, akidai kuwa kamati za uchunguzi zimeundwa.
Kwa wao kudhibiti Al Fasher, RSF imepata kudhibiti majimbo yote matano ya Darfur huko magharibi, kati ya majimbo 18 ya Sudan, huku jeshi la nchi likidhibiti maeneo mengi ya majimbo 13 yaliyobaki kusini, kaskazini, mashariki, na katikati, ikiwemo mji mkuu wa Khartoum.
Eneo la Darfur ni humusi ya nchi nzima ya Sudan, lakini wengi ya raia milioni 50 wa nchi hiyo wanaishi katika maeneo yanayodhibitiwa na jeshi.