Urusi na Ukraine zimeendelea kushambuliana kwa droni na silaha nyingine kwenye maeneo mbali mbali.
Urusi imeshambulia miundombinu ya nishati na bandari Kusini mwa Ukraine katika mji wa Odesa usiku wa kuamkia leo,huku Ukraine nayo ikishambulia kiwanda kimoja ndani ya Urusi.
Shambulio lililofanywa na Urusi dhidi ya miundombinu ya shughuli za kiraia nchini Ukraine limeripotiwa leo na gavana wa Odesa Oleh Kiper ambaye amesema pamoja na juhudi kubwa za kikosi cha jeshi la wanaanga kilicholenga maeneo mengi ya adui, mashambulio ya Urusi yalilenga miundo mbinu ya nishati na bandari.
Moto uliowaka kufuatia mashambulio hayo ya droni za Urusi ulizimwa mara moja na hakuna vifo vilivyoripotiwa.
Wanajeshi wa Ukraine walishambulia kwa droni upande wa Urusi na kuharibu kiwanda cha shughuli za kutengeneza bidhaa zinazotokana na petroli na gesi katika mji wa Sterlitamak, na kusababisha kusitishwa kwa muda kwa shughuli za kiwanda hicho, hata hivyo hakuna aliyejeruhiwa.
Rais Volodymyr Zelensky amezungumzia mapambano yanayoendelea yanayofanywa na nchi yake ndani ya Urusi akisema Moscow inashindwa na hasa katika mji wa Pokrovsk.
“Katika mji wa Pokrovsk adui hajapata mafanikio yoyote katika kipindi cha siku za hivi karibuni. Asilimia karibu 26 mpaka 30 ya hatua zote za kijeshi zinafanyika Pokrovsk.
Na kuhusu matumizi ya mabomu ya kutumia mfumo wa kujiripuwa yenyewe, asilimia 50 yalielekezwa Pokrovsk.Kwahivyo unaweza kuelewa wanajeshi wetu wana kazi ngumu kiasi gani.
Na katika mji huo kuna mamia ya wanajeshi wa Urusi, idadi yao inakadiriwa ni kati ya 260 na 300”
Kyiv imeongeza mashambulizi kwa kutumia droni zinazokwenda masafa marefu na makombora ndani ya Urusi ikilenga viwanda vya kusafisha mafuta, maghala na vituo vya shughuli za usafirishaji ambavyo inasema vinatumiwa na Kremlin kuimarisha uwezo wake wa kijeshi.Urusi yafanya mashambulizi makubwa zaidi ya droni Ukraine
Wizara ya ulinzi wa Urusi hata hivyo katika ripoti yake ya kila siku kuhusu hali ya mapambano imesema mifumo ya ulinzi ya nchi hiyo imeharibu droni 83 zilizoelekezwa kwenye maeneo mbali mbali ya nchi hiyo.Baada ya Uingereza, rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy akutana na Macron, Scholz mjini Paris
Wakati mashambulizi yakiongezeka kuelekea pande zote mbili, mjini Brussels viongozi wa Umoja wa Ulaya wameitaka Ukraine kuharakisha mageuzi ikiwa nchi hiyo inataka kufikia lengo ililojiwekea la kukamilisha mchakato wa kukubaliwa kujiunga na Umoja wa Ulaya kufikia mwishoni mwa mwaka 2028.
Rasimu kuhusu mpango wa kuutanuwa Umoja huo wa Ulaya, imebainishwa kwenye ripoti ambayo imeonekana na shirika la habari la dpa na ambayo imepangiwa kuwasilishwa hii leo Jumanne.