Shirika la Msalaba Mwekundu limesema Jumatatu kuwa liliikabidhi miili hiyo siku moja baada ya miili ya mateka watatu kurejeshwa Israel. Msemaji katika Wizara ya Afya ya Gaza Zaher al-Wahidi, amethibitisha kupokelewa kwa miili hiyo katika hospitali ya Nasser.
Kubadilishana miili ya mateka na Wafungwa kati ya Israel na Hamas kunaashiria hatua nyingine chini ya makubaliano yaliyoratibiwa na Marekani kwa lengo la kuumaliza mzozo mbaya zaidi kati ya Israel na wanamgambo wa Hamas.
Tangu usitishaji vita ulipoanza kutekelezwa wanamgambo wa Hamas wameshakabidhi miili ya mateka 20 kwa Palestina wakati miili ya mateka wengine 8 ikiwa bado iko Gaza.
Israel imekuwa ikiikabidhi Palestina miili 15 kwa kila mwili mmoja wa mateka wake inaokabidhiwa. Kufikia sasa miili ya Wapalestina 270 imesharejeshwa nyumbani tangu makubaliano ya kusitisha vita yalipoanza kutekelezwa.
Guterres aonya kuhusu ukiukwaji wa makubaliano ya kusitisha vita
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres mapema Jumanne ametoa onyo dhidi ya ukiukaji wa makubaliano ya kusimamisha vita Gaza. Ameyasema hayo mbele ya waandishi wa habari pembezoni mwa Mkutano wa pili wa Maendeleo ya Jamii unaofanyika nchini Qatar.
Zaid Guterres amenukuliwa akisema, “Nina wasiwasi mkubwa kuhusu mwendelezo wa ukiukwaji wa makubaliano ya kusitisha vita Gaza. Ni lazima ukiukwaji huu ukome na pande zote husika zinapaswa kuzingatia maamuzi ya awamu ya kwanza ya makubaliano ya amani.”
Guterres ametoa msimamo huo wakati kundi la mataifa ya Kiislamu yenye ushawishi nalo limezitolea wito Israel na Hamas kuzingatia makubaliano ya kusitisha vita na umuhimu wa kuchukua hatua zaidi ili kupata suluhisho la muda mrefu la mzozo huo.
Mawaziri wa Mambo ya Kigeni wa mataifa hayo saba ambayo ni Qatar, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Jordan, Pakistan, Indonesia pamoja na Uturuki ambayo ni mwenyeji wa mkutano huo uliofanyika jana Jumatatu wamesisitiza kuwa njia pekee ya kupata amani ya kudumu ni suluhisho la nchi mbili za Palestina na Israel.
Majadiliano kati ya wanadiplomasia hao yalijikita katika kuimarisha makubaliano ya kusitisha vita kati ya Israel na kundi la Hamas yaliyofikiwa Oktoba 10 pamoja na awamu ya pili ya mpango wa amani wa Rais Donald Trump katika mzozo huo.