Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema Jumatano kuwa Afrika Kusini inapaswa kuondolewa kutoka kundi la G20, na kwamba hatahudhuria mkutano ujao wa kilele nchini humo.

Akizungumza katika Jukwaa la Biashara la Marekani huko Miami, Trump alisema: “Afrika Kusini haipaswi hata kuwa miongoni mwa G20 tena, kwa sababu kilichotokea huko ni kibaya.” Akaongeza kuwa hatapeleka mwakilishi wa Marekani kwenda Afrika Kusini kwa sababu anaamini mkutano wa G20 haustahili kufanyika katika nchi hiyo ya Afrika.

Trump alikuwa akiashiria Mkutano wa Kilele wa G20 unaotarajiwa kufanyika Johannesburg, Novemba 22–23.

G20 ni kambi ya nchi tajiri zaidi kiuchumi na zinazoinukia kiviwanda duniani. Trump amekuwa akiishutumu mara kwa mara Afrika Kusini kwa kutaifisha ardhi na kuwatendea vibaya sana Waafrika Kusini wazungu wanaojulikana kama Afrikanner. Amekuwa akidai kuwa kundi hilo la wazungu linakabiliwa na “ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.”

Katika mwezi Aprili, Trump alisema hapaswi kutarajiwa kwenda Afrika Kusini kwa ajili ya mkutano huo muhimu wa G20 kwa sababu eti wazungu hao wamepokonywa ardhi na wanakabiliwa na “mauaji ya kimbari.”

Mnamo Februari, Trump alitoa Amri ya Utendaji namba 14204, akizielekeza taasisi za shirikisho kurahisisha kuwahamisha Waafrika Kusini wazungu kwenda Marekani kama wakimbizi, akiwataja kama “waathiriwa wa ubaguzi wa rangi usio wa haki.”

Serikali ya Afrika Kusini imekanusha madai ya Trump, ikisema kwamba si ya kweli na hayana msingi wowote.

Mapema wiki hii Serikali ya Afrika Kusini ilikosoa uamuzi wa Marekani wa kuyapa kipaumbele maombi ya hifadhi kutoka kwa Wazungu wa Afrika Kusini, huku ikikanusha  madai ya kuwepo mauaji ya kimbari dhidi yao.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *