Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Masoud Pezeshkian, ameitaka Marekani na nchi za Ulaya kuonesha uaminifu wa dhati endapo zinataka kurejesha imani na Iran.

Katika mazungumzo ya simu aliyofanya Jumatano na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, Pezeshkian alisema ni lazima madola hayo ya Magharibi yaheshimu haki za Iran na yaache kuibebesha masharti yasiyokuwa na mipaka.

Amesisitiza kuwa Iran daima imekuwa tayari kwa mazungumzo na ushirikiano, lakini sasa jukumu la kuthibitisha nia njema lipo kwa upande wa Magharibi.

Amesema: “Sio Iran inayopaswa kuthibitisha ukweli wake na kujenga imani upya. Bali ni Marekani na Ulaya zinazopaswa kudhihirisha uaminifu wao na kuipata tena imani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.”

Rais Pezeshkian ameashiria msimamo thabiti wa Iran kuhusu shughuli zake za nyuklia, unaozingatia fatwa ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Seyyed Ali Khamenei, pamoja na sera ya kiulinzi inayosisitiza kuwa Iran haifuatilii silaha za nyuklia.

Hata hivyo, licha ya msimamo huo, amesema Iran inaendelea kushutumiwa bila msingi na kuwekewa vikwazo vinavyozidi kuongezwa, kwa kisingizio cha kisicho na msingi kuwa inafuatilia mpango wa kutengeneza silaha za nyuklia.

Pezeshkian amesisitiza kwamba changamoto zilizopo zinaweza kutatuliwa kupitia mantiki, mazungumzo, na kuheshimiana, na si kwa vitisho au shinikizo.

Kwa upande wake, Rais Macron alimshukuru Rais Pezeshkian kwa hatua zilizochukuliwa kutekeleza makubaliano yaliyopita, na akaonyesha dhamira ya kuendeleza mwelekeo mpya wa majadiliano kati ya Iran na nchi za Magharibi.

Amesema mazungumzo endelevu ni muhimu ili kujenga uwazi na kuaminiana, hatua itakayowezesha kuondolewa kwa vikwazo na kuimarisha mahusiano ya pande mbili.

Macron amesisitiza: “Ni muhimu mawasiliano yetu yaendelee kwa lengo la kujenga uwazi na kuaminiana, ili tuweze kufikia makubaliano, na sambamba na kuondoa vikwazo, kuboresha na kupanua mahusiano ya pamoja.”

Kabla ya mashambulizi ya angani ya Marekani na Israel mwezi Juni dhidi ya Iran na baadhi ya miundombinu yake ya nyuklia, Tehran na Washington zilikuwa zimefanya duru tano za mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kufufua makubaliano mbadala ya lile la mwaka 2015.

Hata hivyo, Marekani na washirika wake wa Ulaya wameendelea kusisitiza kwamba makubaliano yoyote mapya yazingatie si tu shughuli za nyuklia za Iran, bali pia mpango wake wa makombora ya masafa marefu.

Tehran imekataa msimamo huo mara kwa mara, ikisisitiza kuwa uwezo wa kijeshi ni suala lisiloweza kujadiliwa.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *