Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetoa mjibizo kwa matamshi ya Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu kuanza tena nchi hiyo kuzifanyia majaribio silaha zake za nyuklia.

Amir Saeed Iravani, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa, siku ya Jumanne, alimwandikia barua Rais wa Baraza la Usalama pamoja na Katibu Mkuu wa umoja huo, akitoa mjibizo kwa matamshi ya Rais wa Marekani Donald Trump na vitisho alivyotoa kuhusiana na silaha za nyuklia, na akasema, matamshi hayo “yanatia wasiwasi mno”.

Iravani alibainisha kwa kusema: “matamshi haya ni tishio kubwa kwa amani na usalama wa kimataifa na ni ukiukaji wa wazi wa majukumu unaofanywa na Marekani kwa mujibu wa sheria za kimataifa.”

Amir Saeed Iravani, Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa,

Katika barua yake hiyo, Iravani ameendelea kueleza: “mnamo tarehe 29 Oktoba, Rais wa Marekani alitangaza hadharani kwenye mitandao ya kijamii, kwamba ameiamuru wizara ya vita ya Marekani ‘ianze kuzifanyia majaribio silaha zake za nyuklia kwa mlingano wa usawa na mataifa mengine yenye nguvu za nyuklia,’ na akabainisha kwamba, ‘mchakato huo utaanza mara moja.’ Baadaye, mnamo Oktoba 31, katika mahojiano na programu ya Dakika 60 ya CBS alitamka kuwa, Marekani peke yake ‘ina kiwango cha silaha za nyuklia zenye uwezo wa kuiripua dunia mara 150.’

Mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amefafanua kwa kusema: “kauli hizi za upayukaji, na uropokaji wa kimihemko uliofanywa na rais wa nchi yenye silaha za nyuklia ni kitisho cha dhahiri cha nia ya kutumia silaha za nyuklia na ni tangazo la wazi la kusudio la kuanza tena kufanya majaribio ya nyuklia. Kitendo hiki ni ukiukaji wa wazi wa majukumu yanayoilazimu Marekani chini ya Kifungu cha VI cha ‘Mkataba Unaopiga Marufuku Uenezaji Silaha za Nyuklia’ unaohusiana na uchukuaji hatua madhubuti za kupunguza silaha za nyuklia, na kinapingana moja kwa moja na lengo na madhumuni ya ‘Mkataba wa Kupiga Marufuku Kikamilifu Majaribio ya Nyuklia’, ambao Marekani imeusaini, na vilevile kinakinzana dhahir shahir na ahadi iliyotoa nchi hiyo ya kutekeleza agizo la kusitisha majaribio ya nyuklia.”

Msimamo rasmi iliotangaza Iran kuhusu muelekeo mpya wa nyuklia ulioonyeshwa na Trump unafahamika mantiki yake tukizingatia vitisho vya mara kwa mara ambavyo rais huyo wa Marekani amekuwa akivitoa dhidi ya mpango wa nyuklia wa Iran wenye malengo ya amani. Baada ya kushirikiana na Israel katika kuvishambulia vituo vya nyuklia vya Iran wakati wa vita vya siku 12 vilivyoanzishwa na utawala huo wa Kizayuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu; tangu wakati huo, Trump hajaacha kutoa vitsiho, akikumbusha kila mara kwamba atachukua hatua za kijeshi dhidi ya Iran ikiwa itaanza tena shughuli zake za nyuklia. Wakati alipohutubia hafla ya maadhimisho ya kuasisiwa Jeshi la Wanamaji la Marekani, Trump alisema: “tulikuwa tumefanya mazoezi kwa muda wa miaka 22 ya kushambulia vituo vya nyuklia vya Iran… Ikiwa Iran itaanzisha tena mpango wake wa nyuklia, hatutasubiri kwa muda mrefu kuishambulia tena Iran”.

Haya yanajiri katika hali ambayo, rais huyo mtatanishi wa Marekani, amechukua hatua inayokiuka waziwazi majukumu ya kimataifa iliyojifunga nayo nchi yake, kwa kutangaza kwamba Washington itaanza tena kufanya majaribio ya nyuklia, hatua ambayo imezua mvutano kimataifa na kuzusha hofu ya kuongezeka ushindani wa silaha za nyuklia. Uamuzi huo ni sawa na kubadilika kikamilifu sera ya muda mrefu ya Marekani. Itakumbukuwa kuwa, jaribio la mwisho la nyuklia la Marekani lilifanyika Septemba 23, 1992, yaani muda mfupi kabla ya Rais wa wakati huo Mrepublican George H. W. Bush kusimamisha ufanyaji wa majaribio hayo, sambamba na kufikia tamati enzi za Vita Baridi.

Inavyoonekana, dunia inakaribia kuingia kwenye awamu mpya ya ushindani wa nyuklia wenye gharama kubwa. Hivi sasa, na kwa uamuzi wa nyuklia uliotangazwa na Trump, uwezekano wa kurudi tena kwenye mashindano ya uundaji wa silaha hizo ulioshuhudiwa katika miongo iliyopita, umeongezeka. Madola yenye nguvu za nyuklia, hususan Russia na China, yanaweza kuitumia hatua ya Marekani ya kuanza tena kufanya majaribio ya nyuklia ili nayo pia kuliweka suala hilo kwenye ajenda zao; na baada ya hapo, njia itakuwa imefunguliwa kwa Ufaransa na Uingereza ili nazo pia zianze kufanya majaribio ya silaha za nyuklia. Sambamba na hayo, nchi zingine zinazomiliki silaha za nyuklia zitapata kisingizio zinachohitaji ili kufanya majaribio ya silaha hizo angamizi ambayo yatakuwa na athari mbaya sana kwa mazingira.

Viongozi wa nchi nne zinazomiliki silaha za nyuklia

Kimsingi hasa ni kwamba, moja ya sababu muhimu za kuanzishwa na kutekelezwa Mkataba wa Kupiga Marufuku Kikamilifu Majaribio ya Nyuklia ilikuwa ni athari za uharibifu ambao wakati mwingine hauwezi kufidika, unaosababishwa na majaribio ya nyuklia kwenye mazingira yanapofanyiwa majaribio hayo, au hata maeneo yaliyo mbali na hapo. Uchafuzi wa udongo na maji, uchafuzi wa angahewa na uwepo wa mionzi ya nyuklia na athari zake hatari sana kwa viumbe vyote hai, ndivyo hatimaye vilivyopelekea kutolewa agizo la kukomesha ufanyaji majaribio ya nyuklia katika mazingira halisi na kuhamishia majribio hayo kwenye mazingira ya maabara. Lakini hivi sasa, na baada ya tangazo lililotolewa na Trump, kengele imeshalia ya kuanzishwa tena uharibifu na maangamizi ya sayari ya dunia.

Kwa ujumla, kuanza tena Marekani kufanya majaribio ya nyuklia kunaweza kuwa na matokeo hasi makubwa ikiwa ni pamoja na:

– Kuongezeka mvutano kati ya madola yenye nguvu za nyuklia kama vile Russia, China na Marekani.

– Kudhoofisha mikataba ya udhibiti wa silaha na kuongeza uwezekano wa nchi kujiondoa katika mikataba ya kimataifa.

– Kuzichochea nchi za kikanda kwa kuzifanya zistawishe mipango yao ya nyuklia.

– Kuongeza hatari ya kuzuka mapigano ya kijeshi kwa kutumia silaha za maangamizi ya halaiki.

– Na kuongezeka kwa kiwango kikubwa uchafuzi wa kinyuklia ndani na karibu na maeneo ya majaribio bali hata kwenye maeneo ya mbali.

Kwa kuzingatia muelekeo mpya wa nyuklia ulioonyeshwa na Trump, jukumu la jamii ya kimataifa katika kudhibiti mgogoro na kuzuia kuenea silaha za maangamizi ya halaiki linakuwa na umuhimu mkubwa, zaidi ya ilivyokuwa huko nyuma. Na ni kwa kupitia ushirikiano, kuwepo na uwazi na diplomasia ndipo itawezekana kuzuia kurejea tena kwenye enzi za giza za Vita Baridi…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *