Tanzania yadaiwa kuitupa kiholela miili ya waandamanajiTanzania yadaiwa kuitupa kiholela miili ya waandamanaji

Tanzania kwa hivi sasa iko kwenye kiza kinene cha simanzi kufuatia mauaji yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi nchini humo. Maandamano makubwa ya vurugu yaliigubika nchi hiyo kwa siku kadhaa wakishuhudiwa vijana walioingia mitaani kuupinga uchaguzi huo uliomuingiza madarakani Samia Suluhu Hassan na ambao waangalizi wa kigeni waliutaja kuwa ni zoezi lililoshindwa kufikia viwango vya kidemokrasia kwasababu wapinzani wakuu walizuiwa kushiriki.

Mamlaka za Tanzania zilitangaza amri ya kuwataka wananchi kutotoka nje huku vikosi vya usalama vikiingia kazini kuwaandama waandamanaji kwa kuwafyetulia risasi za moto na mabomu ya machozi. Chama kikuu cha upinzani CHADEMA kimedai kwamba zaidi ya watu 1000 waliuwawa na siku ya Jumanne chama hicho kikasema kwamba vikosi vya usalama vinajaribu kutafuta njia za kuficha ukubwa wa mauaji yaliyotokea kwa kuchukuwa hatua za kuitupa  kwa siri miili ya waliouwawa.

Upinzani wasema Rais Samia hajutii mauaji ya waandamanaji

Mamlaka za serikali hazijatowa tamko lolote la kuzungumzia madai ya Chadema. Deogratius Munishi ambaye ni miongozi mwa viongozi waandamizi ndani ya Chadema amezungumzia suala hilo la mauaji na zaidi akataja kuhusu namna wanavyosikitishwa na msimamo unaochukuliwa na mamlaka za serikali kuhusu kilichotokea akimnyooshea kidole rais Samia ambaye amemtaja kama mtu asiyejutia kilichotokea.

Tansania Dodoma 2025 | Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan
CHADEMA yasikitishwa na msimamo unaochukuliwa na mamlaka za serikali kuhusu kilichotokea ikiimnyoshea kidole cha lawama rais Samia ambaye imemtaja kama mtu asiyejutia kilichotokea.Picha: Tanzania State House

“Rais Samia hana majuto kwa kilichotokea. Hajali kuhusu idadi ya Watanzania waliouawa na vikosi vya usalama chini ya mamlaka yake na hiki ni kitu kinachowaumiza zaidi Watanzania.”

Kiongozi mwingine mwandamizi wa Chadema Brenda Rupia alizungumzia pia kuhusu namna masikitiko yalivyowajaa Watanzania akisema mioyo ya raia inavuja damu hivi sasa na kilichotokea ni hali mpya kabisa kwa Watanzania. Duru za kidiplomasia zinasema kwamba ziko ripoti za kuaminika zinazoonesha kwamba mamia na pengine hata maelfu wameuwawa, na vifo hivyo vimesajiliwa katika mahospitali na zahanati kote nchini Tanzania.

Shirika la Human Rights Watch siku ya Jumanne lililaani hatua ya kuandamwa waandamanaji na ikatowa mwito kwa mamlaka za nchi hiyo kusitisha matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji na kuchukuwa hatua za kuhakikisha uwajibikaji wa vikosi vya usalama. Shirika hilo lilisema watu mbali mbali nchini humo wameshuhudiwa polisi wakiwaua kwa kuwapiga risasi watu. Oryedm Nyeko ni mtafiti mwandamizi tawi la Afrika katika shirika la Human Rights Watch.

Ghasia za baada ya uchaguzi Tanzania,Mtihani kwa rais Samia

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

“Zimekuweko ripoti za kuuawa kwa zaidi ya watu 1000. Hiki ndicho wamekuwa wakikisema upinzani. Ni vigumu kuthibitisha idadi hii na hasa katika kipindi cha siku chache zilizopita kutokana na kutokuweko kwa mtandao wa Intanet nchini,na taarifa nyingi zilikuwa zikisambazwa  lakini ni vigumu kujuwa kwahakika ikiwa idadi ya vifo inayotolewa ni sahihi au la.Kwahivyo nafikiri katika siku chache zijazo vizingiti vya kuzuiwa intanet vikiondoka kikamilifu ,watu watakuwa na uwezo wa  kupata hasa kujuwa  kile kilichotokea katika kipindi cha wiki nzima,” alisema Oryedm Nyeko.

Uingereza, Norway na Canada zimetaja juu ya kuweko ripoti za kuaminika kuhusu idadi kubwa ya waliouawa. Hata Kanisa Katoliki limesema watu waliuliwa kwa mamia japo kanisa hilo halikuweza kuthibitisha idadi hasa inayotajwa. Huku rais wa Chama cha wanasheria Tanganyika , Tanganyika Law Society  Bonifas Mwabukusi akisema waziwazi kwamba zaidi ya watu 1,000 wameuawa kwa mujibu wa taarifa za matukio zilizopokelewa na chama hicho na kwamba wako kwenye mchakato wa kukusanya ripoti itakayopelekwa pia kwa mashirika ya Kimataifa ya kisheria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *