Dar es Salaam. Kuna uwezekano mkubwa mshambuliaji Clement Mzize akazikosa Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 kutokana na upasuaji wa goti ambao amefanyiwa utakaomuweka nje kwa zaidi ya miezi miwili.

Mzize ambaye ni miongoni mwa wachezaji nyota wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ tayari ameshakosa mechi mbili zilizopita za timu hiyo na sasa anaelekea kuzikosa fainali za AFCON 2025 ambazo zitafanyika Morocco kuanzia Desemba 21 mwaka huu hadi Januari 18 mwakani.

Ofisa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe amesema kuwa mshambuliaji huyo amelazimika kufanyiwa upasuaji huo kutokana na usugu wa majeraha ya goti ambayo yamekuwa yakimsumbua kwa muda mrefu.

“Mara ya mwisho tunazungumza tuliwapa taarifa ya mchezaji Clement Mzize ambaye kimsingi ndiye mchezaji pekee mwenye majeraha kwenye kikosi ambacho tupo nacho msimu huu.

“Baada ya kufanyika vipimo na ushauri wa jopo la madaktari wa klabu yetu wakishirikiana na benchi la ufundi na mchezaji mwenyewe (Mzize), tulifikia kukubaliana mchezaji huyu akafanyiwe upasuaji kwa sababu alikuwa anapona kidogo na anarudi uwanjani na anapata majeraha tena.

“Tutamkosa Mzize uwanjani kwa kipindi cha wiki nane hadi 10 huku madaktari wakiendelea kukagua kwa karibu hali yake,” alisema Ally Kamwe.

Wakati Mzize akitarajiwa kuwa nje kwa muda usiopungua wiki nane, zimebaki wiki saba tu kabla ya kuanza kwa fainali za AFCON 2025 ambazo Taifa Stars itakuwa katika kundi C pamoja na timu za Tunisia, Uganda na Nigeria.

Mzize ni miongoni mwa wachezaji muhimu katika kikosi cha Taifa Stars ambacho amekuwa miongoni mwa nyota wanaocheza mara kwa mara.

Mshambuliaji huyo alithibitisha hilo katika fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wanaocheza Ligi za Ndani (CHAN) 2024 ambapo aliibuka mfungaji bora wa Taifa Stars baada ya kupachika mabao mawili.

Akizungumzia majeraha ya Mzize, mshambuliaji wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Makumbi Juma ‘Homa ya Jiji’ amesema kuwa ni pigo kwa timu hizo mbili.

“Mzize ni mchezaji muhimu katika kikosi chetu cha Yanga maana yuko vizuri katika kutumia nafasi lakini hata kwa Taifa Stars tunamhitaji sana hasa ukizingatia tuna mashindano magumu mbele,” alisema Homa ya Jiji.

Katika kikosi cha Yanga, nafasi ya Mzize imekuwa ikichezwa na Prince Dube au Andy Boyeli lakini katika Taifa Stars wapo Mbwana Samatta, Paul Peter na Selemani Mwalimu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *