
Watu wasiopungua 90 wamefariki dunia na wengine 75 hawajulikani walipo hadi sasa kufuatia kimbunga cha Kalmaegi kuathiri maeneo ya kati ya Ufilipino jana Jumatano.
Miongoni mwa waliofariki dunia ni watu sita waliouawa wakati helikopta ya jeshi la anga la Ufilipino ilipoanguka katika jimbo la kusini la Agusan del Sur siku ya Jumanne.
Jeshi la Ufilipino limebainisha kuwa, wafanyakazi wa huduma wa uokoaji walikuwa njiani kutoa msaada wa kibinadamu katika majimbo yaliyokumbwa na kimbunga Kalmaegi.
Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa ya Ufilipino imeripoti kuwa, kimbunga hicho kilipiga katika jimbo la magharibi la Palawan hadi katika Bahari ya China Kusini kabla ya saa sita mchana jana Jumatano sambamba na kuvuma upepo mkali wa hadi kilomita 180 kwa saa.
Bernardo Rafaelito Alejandro IV, Naibu Mkuu wa Ofisi ya Ulinzi wa Raia na maafisa wa uongozi wa majimbo wa Ufilipino wameeleza kuwa vifo vingi vimeripotiwa katika jimbo la kati la Cebu, ambalo Jumanne wiki hii lilikumbwa na kimbunga cha Kalmaegi na kusababisha mafuriko na kujaa maji katika mito.
Shirika la Msalaba Mwekundu la Ufilipino limepokea simu nyingi kutoka kwa watu waliohitaji kuokolewa katika jimbo la Cebu
Wakati huo huo watu wengine 62 hawajulikani walipo katika maeneo ya kati Negros Occidental na Negros Oriental yanayopatikana karibu na Cebu.
Pamela Baricuatro Gavana wa jimbo la Cebu amesema kuwa wamefanya kila wawezalo ili kukabiliana na kimbunga cha Kalmaegi hata hivyo kuna mambo yasiyotarajiwa kama vile mafuriko ya ghafla yanayosababishwa na mvua kubwa.