Manchester, England. Manchester City imzeidi kujiweka pazuri kuelekea hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuichapa Borussia Dortmund 4-1 kwenye Uwanja wa Etihad, usiku wa jana, huku Phil Foden akionyesha ubora wa hali ya juu unaoweza kumrudisha kwenye kikosi cha England.

Foden alifunga mabao mawili, huku Erling Haaland akiendeleza rekodi yake ya kufunga kwenye michuano mikubwa kwa bao lake la 27 msimu huu. Mashabiki wa City walionyesha bango lenye maandishi “Erling The Great” likimwonyesha kama shujaa.

Ushindi huu ni wa pili mfululizo nyumbani, City sasa ipo katika nafasi nzuri ya kufuzu hatua ya mtoano. Mechi zijazo itakutana dhidi ya Bayer Leverkusen na Galatasaray inaweza kuwa fursa ya kufikia nane bora bila kupitia hatua ya mchujo.

Ushirikiano wa Foden na Reijnders watia matumaini

Kipindi chote cha kwanza, uelewano wa hali ya juu kati ya Tijjani Reijnders na Foden uliipa City ubunifu zaidi. Mara mbili Reijnders alimpasia Foden katika eneo la hatari, na mara zote kiungo huyo wa England akamalizia kwa ustadi mkubwa.

Kwa ubora huu, kocha wa England, Thomas Tuchel atalazimika kufikiria mara mbili kabla ya kumuacha Foden kwenye kikosi kitakachotajwa Ijumaa.

Rodri bado kitendawili kwa Guardiola

City ilicheza bila kiungo wake muhimu Rodri, ambaye bado anasumbuliwa na maumivu licha ya kurejea benchi hivi karibuni. Guardiola alisema mchezaji huyo “hajisikii sawa kabisa”

Kwa sasa, Nico González anaendelea kuziba pengo hilo vyema, akionyesha uimara wa kiufundi na nidhamu kubwa uwanjani.

Donnarumma mlinzi wa uhakika langoni

Kama kuna eneo linalotia matumaini zaidi, basi ni langoni. Gianluigi Donnarumma alionyesha kwanini Guardiola amemwamini.

Alizuia kwa ustadi shuti la Karim Adeyemi, na baadaye akamnyima Serhou Guirassy bao la wazi. Bila tulivu wake, mchezo huu ungeweza kubadilika kabisa.

Savinho bado anatisha

Kinda wa Kibrazil Savinho alipata nafasi ya kuanza baada ya mechi mbaya dhidi ya Bournemouth, na alionyesha kasi na ujanja wa hali ya juu. Aliwasumbua mabeki wa Dortmund kila alipokuwa na mpira, hasa Daniel Svensson, aliyelazimika kumwangusha na kupewa kadi.

Rayan Cherki aliingia dakika za mwisho na kufunga bao la nne kwa ustadi, akionyesha nini kinachotakiwa kwenye kiwango cha juu.

Mechi nyingine za Ligi ya Maboingwa Ulaya zilizopigwa jana ilishuhudiwa Chelsea ikilazimishwa sare ya 2-2 ugenini dhidi ya Qarabag sawa na Barcelona iliyolazimishwa sare ya 3-3 ugenini dhidi ya Club Brugge wakati Ajax ikichapwa kwenye uwanja wake wa nyumbani na Galatasaray.

Newcastle United iliibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Athletic Bilbao, Inter Milan ikaichapa Kairat Almaty mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Giussepe Mezza, Pafos ikaifunga 1-0 Villarreal sawa na Bayer Leverkusen iliyoilaza 0-1 Benfica wakati Marseille nayo ikipoteza kwa bao 1-0 nyumbani dhidi ya Atalanta.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *