Dar es Salaam. Vurugu zilizosababishwa na maandamano yaliyotokea Oktoba 29, 2025 hazijaacha maumivu tu kwa baadhi ya wasanii nchini kufuatia uharibifu wa mali zao na biashara, bali pia zimechochea hali ya sintofahamu kati mashabiki na kundi hilo.
Baadhi ya wasanii waliokutana na kadhia hiyo ni mwanamuziki Zuwena Mohammed ‘Shilole’ ambaye mgahawa wake ulichomwa moto, William Lyimo ‘Billnass’ duka lake lilichomwa, naye Juma Mkambala ‘Jux’ duka lake lilivamiwa na kufanyiwa uharibifu ikiwamo kuvunjwa vioo.
Mvutano wa pande mbili kati wasanii na mashabiki ulianza kuonekana kabla ya tukio hilo lililoacha hasara kwa wasanii.
Kwa kile kinachoelezwa kwa kundi hilo, ni kwamba licha ya ushawishi wake, mara nyingi halipo pamoja na wanajamii zinapotokea changamoto ikiwamo matukio ya utekaji na mauaji.
Kupitia mitandao ya kijamii, mashabiki wameonesha hasira yao dhidi ya wasanii huku kukiwa na kundi linaloonesha waziwazi kufurahishwa na vitendo vya uharibifu wa mali za wasanii hao.
Pia, wapo wanaochochea uharibifu zaidi kufanyika kwa wengine.
Kwa wafuatiliaji wa mitandao ya kijamii kuanzia Novemba 3, 2025 siku ambayo mawasiliano ya intaneti yalirejea, wasanii walitumia kurasa zao kutoa pole kwa familia za watu waliopoteza maisha kutokana na vurugu zilizotokea siku ya uchaguzi.
Kati ya wasanii waliojitokeza kuzungumzia hilo ni Steve Nyerere kwa kuandika: “Kama Mtanzania nichukue fursa hii kuwapa pole Watanzania wote. Taifa hili sifa yake kubwa ni amani na mshikamano, tumepoteza vijana wetu. Lakini wakati tunalia lazima tujiulize huu ndiyo utamaduni wetu? Nini kimetufanya tufike hapa na wakati tunajiuliza tujue kila Mtanzania ana jukumu la kurudisha heshima na tunu ya Taifa letu.
“Ndugu zangu huu sio wakati wa kunyoosheana vidole. Ni wakati wa kuungana na kumwambia shetani sisi ni wamoja kwa masilahi mapana ya Taifa letu. Umoja na mshikamano wa Taifa letu ubaki kama alama na tunu ya Taifa.”
Kupitia ukurasa wake wa Instagram msanii wa vichekesho, Masatu Ndaroameandika ujumbe ulioonesha kuumizwa kwake na namna kundi la wasanii linavyopitia maswahibu kwa sababu ya kuonesha upande wao kama ilivyo kwa wananchi wengine.
“Hakuna kitu kigumu kama kuwa msanii, kabla ya kutuhukumu fikiria kwanza msanii naye ni raia kama raia wengine hana mamlaka yoyote. Ni kipi tulichowakosea sisi wasanii, mfano mimi anayejua kosa langu aseme nimewakosea nini. Watu maarufu waliothirika na itikadi za vyama baada ya kupata madhara wananchi walifanya nini kwa familia zao.”
“Kwa kutambua maisha tunayotokea na watu wanaotutegemea tufuate sheria, taratibu na kanuni za nchi. Ila kwa wananchi tunaonekana kama hatujitambui na kuhukumiwa. Mnachotakiwa kutambua hakuna msanii hajui faida ya wananchi.”
Akionesha machungu kwa kile kilichotokea kwenye biashara yake Shilole, alitoa barua ya wazi akieleza kuwa kurudishiana maumivu si utu.
Shilole ameandika: “Kwanza, nitoe pole za dhati kwa wote waliofikwa na misiba, majeraha au hasara kutokana na vurugu zilizotokea. Kurudishiana maumivu si utu, wala si msingi wa Taifa letu. Tofauti za kisiasa hazitufanyi tuache kuwa jamii moja, kwani kabla ya itikadi, sisi ni binadamu na ni Watanzania. Mimi ni mhanga wa fujo hizo, ofisi yangu imechomwa na mali zangu zimeteketea.
“Wapo wanaoonekana kufurahia, wakidai nilistahili kwa sababu ya msimamo wangu wa kisiasa. Lakini ukweli ni huu, sijawahi kumtukana mtu, sijawahi kumdhuru mtu nimekuwa tu muumini wa siasa ninayoiamini kupitia chama changu CCM.”
Msanii huyo aliyetamba na nyimbo kama Sitaki Mazoea, Nakomaa na Kijiji, Lawama na nyingine nyingi, katika barua hiyo pia ameeleza kuwasamehe waliohusika kuhari ofisi yake.
“Kwa hivyo, wakati huu si muda wa kutafutana mchawi, wala kushindana kutupiana lawama. Ni wakati wa busara. Nawabariki na kuwasamehe wote waliohusika katika uharibifu wa biashara yangu huku wakiwa wamedhamiria kunirudisha nyuma.
“Muhimu ni kwamb, Mwenyenzi Mungu ameendelea kuniruzuku uhai basi ninaamini mali zinaweza kurejeshwa kwa juhudi na kupambana pasipo kukata tamaa, lakini pumzi ya uhai haina mbadala,” ameandika msanii huyo.
Kwa upande wake, Jux amehamasisha maombi kwa Taifa huku akimuomba Mungu kuwatia nguvu waathirika wote.
Haikuishia hapo naye msanii Ally Saleh ‘Alikiba’ ameomba radhi kwa mashabiki wake huku akitoa pole
“Poleni ndugu zangu Watanzania na ninawaomba msamaha kwa kuwakwaza,”ameandika Alikiba.
Hata hivyo, hatua hiyo haikupokewa vyema na baadhi ya wananchi wanaowafuatilia kwenye mitandao hiyo. Badala yake waliwashambulia wakiwatuhumu wasanii kwa kutokemea maovu yanayosibu jamii.
Kwa nini hasira za mashabiki?
Akitoa maoni yake kuhusu hicho kinachoendelea kati ya wasanii na mashabiki, mwalimu John Magoda amesema huenda malalamiko ya wasanii ni matokeo ya kusahau mada ya sanaa ya kidato cha kwanza lakini pia wamesahau kabisa mada ya fasihi kidato cha tatu.
“lko hivi hakuna mwanajamii ambaye anampangia msanii kuwa chama gani, hilo wanatakiwa kuelewa. Ila ukishakuwa msanii wewe ni mali ya jamii na unatakiwa kusimama na jamii yako hata kama uko chama chochote kile.
“Ndio maana katika harakati za kudai uhuru wa nchi hii unaona mchango mkubwa wa wasanii kwa makundi yote kuanzia waimbaji, wachoraji hadi waandishi wa vitabu walishiriki kikamilifu kwa maslahi mapana ya taifa letu,” amesema Magoda.
Amesema kwa sababu hiyo ukishakuwa msanii, jamii inapopata changamoto unatakiwa kusimama nayo kwa kuungana nao katika kupaza sauti, mambo mabaya katika jamii yao bila kujali chama alichopo msanii.
“Hata hivyo, wasanii wengi waliamua kukaa kimya kabisa kama hakuna kitu hata kidogo. Hata katika mambo ambayo yalihitaji sauti yenu au hata post zenu tu hizo ndio ziliwatia hasira wananchi wengi na wala sio kushiriki kampeni au kuwa chama fulani so msijifiche katika kichaka cha chama fulani cha siasa.
“Kwa sasa wasitizame walipodondokea ila watazame walipojikwaa na waamue kuanza upya kwa mustakabali chanya wa Taifa letu. Kuwa msanii sio jambo jepesi, jamii haiwalaumu kwa sababu wako chama fulani maana wanajua mna uhuru wa kuwa upande wowote ila wanasema katika mambo ya kijamii wanakuwa kimya,” amesema Magoda.