Kilio cha watanzania na hasa waliopoteza ndugu na jamaa zao kufuatia vurugu zilizotokea kinaendelea kusikika japo kimyakimya na kwa khofu kubwa.
Lawama za mauaji yanayotuhumiwa kufanywa na vikosi vya usalama zinasikika kutoka makundi mbali mbali, tangu Umoja wa Mataifa, masharika ya kutetea haki za binadamu hadi chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania CHADEMA ambacho kimedai idadi ya waliouawa wanaweza kufikia zaidi ya watu 1,000. Rais Samia Suluhu Hassan ndiye kiongozi mkuu wa majeshi nchini Tanzania na bila shaka mwenyekiti wa chama tawala kinachoiongoza nchi hiyo kwa zaidi ya miaka 50.
Chini ya uongozi wake kabla ya uchaguzi huu, kumetokea ukandamizaji mkubwa dhidi ya wapinzani wake wa kisiasa ambapo miongoni mwa ukandamizaji huo ni pamoja na kumzuia kiongozi wa chama kikuu cha upinzani Chadema Tundu Lissu kushiriki uchaguzi, kwa kufunguliwa mashtaka ya uhaini baada ya kutowa mwito wa kudai mabadiliko ya sheria za uchaguzi.
Hivi sasa wakati rais Samia akiwa ndiye anayelengwa zaidi na hasira za Watanzania, wakosoaji wanasema hayuko peke yake, ana washirika na kwa kiasi kikubwa sio yeye mwenye usemi mkubwa.
v
Jakaya Mrisho Kikwete ndiye rais pekee wa zamani wa Tanzania aliyeko hai, bado ameendelea kuwa na ushawishi mkubwa katika siasa za nchi hiyo tangu alipomaliza muda wake mwaka 2015 na yeye alikuwa chachu ya mageuzi ya uongozi alipofariki akiwa madarakani rais John Pombe Magufuli mnamo mwaka 2021 na kuingia Samia Suluhu Hassan.
Watanzania wengi wanamuona Kikwete kama mtu aliyecheza nafasi kubwa nyuma ya pazia kuunga mkono kuingia kwa Samia na wanamkosoa juu ya machafuko yaliyotokea. Kikwete bado hajasema chochote kujibu tuhuma za namna hiyo hadharani. Mwanasheria wa masuala ya haki za binadamu Tito Magoti amesema Kikwete pia anatazamwa kama mtu anayesimamia maslahi ya kibiashara ya wageni akihakikisha anaendeleza uthabiti wa kisiasa. Lakini yuko pia makamu wa rais Emmanuel Nchimbi aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani na katibu mkuu wa CCM aliyemaliza muda wake.
Yeye na Samia waliapishwa Jumatatu kuiongoza nchi. Nchimbi anatazamwa kama mtu mwenye mtazamo halisi wa CCM, ambaye ana nafasi nzuri ya uwezekano wa kumrithi Samia muhula wake wa miaka mitano utakapomalizika. Yuko pia lakini mtoto wa kiume wa rais Samia ambaye anatajwa kwa hakika ndiye mshauri wake mkuu, Abdul Halim Hafidh Ameir.
Hadi sasa Humprey Polepole hajulikani aliko
Wakati huyu hashikilii nafasi yoyote rasmi katika serikali ya Samia, baadhi ya wakosoaji wanadai alikuwa mpanga mikakati mkubwa wa mpango huu wa kuwaandama waandamanaji, hii ikiwa ni kwa mujibu wa William Farmer, mtafiti wa masuala ya ushauri kuhusu Afrika.
Humprey Polepole, aliyekuwa balozi wa Tanzania nchini Cuba na kiongozi mwandamizi wa zamani wa CCM alipotezwa na hadi sasa haijulikani aliko tangu kuchukuliwa kutoka nyumbani kwake mwezi uliopita baada ya kumkosoa rais Samia na kutuhumu kwamba Abdul alikuwa ndiye mkuu asiye rasmi wa idara ya ujasusi. Abdul hajawahi kujibu tuhuma hizo hadharani.
Pia, aliyewahi kuwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda naye ni mmoja wa wanasiasa wanaotajwa kuwa na usemi ndani ya CCM.
Kwa mujibu wa William Farmer mtafiti kutoka shirika linaloshughulikia masuala ya kutoa ushauri kuhusu Afrika, lenye makao yake London anasema kuna uwezekano mkubwa kwamba Makonda akapewa nafasi ya juu ya uongozi katika serikali ijayo. Na itakumbukwa Marekani iliwahi kumuwekea vikwazo Makonda kwa tuhuma za kuhusishwa na ukandamizaji wa wanasiasa wa upinzani.