Akiwa kwenye kituo cha mwisho cha ziara yake Afrika mjini Huambo nchini Angola, Rais Steinmeier amesema mradi wa reli wa Lobito ni wa kimkakati wenye umuhimu mkubwa kiuchumi. Mradi huo unakusudia kuunganisha mji wa pwani wa Lobito na mikoa yenye utajiri wa rasilimali kusini mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hadi Zambia.
Aidha Steinmeier amesema kwa kuwa kampuni ya barani Ulaya ilishinda zabuni ya mradi huo, makampuni ya Ujerumani na Ulaya kwa Ujumla yana nafasi kubwa ya kufanya uwekezaji.
Ametoa kauli hiyo siku mbili baada ya Rais wa Angola João Lourenço kutoa wito kwa Ujerumani kufanya uwekezaji zaidi nchini Angola. Steinmeier anahitimisha ziara yake ya siku mbili Angola kwa kuutembelea mji wa Huambo ambao ni watatu kwa ukubwa nchini humo.
Steinmeier ahitimisha ziara yak mradi wa kutegua mabomu ya ardhini
Ameutembelea mradi wa kuondoa mabomu ya ardhini ambayo bado hayajalipuka na kituo cha kuwasaidia waathiriwa wa mabomu mjini Huambo.Kituo hicho kilianzishwa wakati wa ziara ya mke wa mwanamfalme wa Uingereza wa wakati huo marehemu Princess Diana mnamo mwaka 1997.
Mabomu ya kutegwa ardhini wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyokwisha mwaka 2002 bado yanahatarisha maisha ya raia.
Rais huyo wa Ujerumani ndiye wa kwanza wa taifa hilo kuitembelea Angola ambapo ziara yake imelenga kuonesha msimamo wa nchi hiyo kama mshirika muhimu wa kisiasa na kiuchumi.
Angola kwa sasa inashikilia uenyekiti wa kupokezana wa Umoja wa Afrika wenye mataifa 55 wanachama. Nchi hiyo ni mzalishaji wa nne kwa ukubwa wa madini ya almasi na ina hifadhi kubwa ya malighafi muhimu ambazo sekta ya viwanda ya Ujerumani inazihitaji.
Kabla ya kuhitimisha ziara yake nchini Angola, Steinmeier aliyatembelea mataifa ya Misri na Ghana. Alipokuwa Ghana, alitangaza kuwa nchi yake itatoa msaada wa dola milioni 69 za Kimarekani kwa ajili ya maendeleo nchini humo. Miradi iliyolengwa ni ya nishati jadidifu, viwanda na miradi ya kidijitali.