Jijini Kisumu, eneo la Milimani mkabala wa mtaa wa mabanda wa Nyalenda, ni Shule ya Msingi ya Greenview, ndio walipo wavumbuzi wa pipa la kisasa la kutupia taka linalojifungua bila kuguswa ila kwa kusogelea sehemu iliyowekwa mtambo maalum, maarufu kama ”sensor” yenye uwezo wa kuhisi kabla ya mguso au kiwiliwili ili kujifungua. Pipa hili maalum ni lenye rangi ya buluu, kijani kibichi na mfuniko wenye rangi nyeusi na lenye maandishi ya uvumbuzi wa kujifungua pamoja na jina la shule la wasichana hao.
Wanafunzi hao wanaelezea kilichochangia ubunifu huu kwamba ni kutokana na yaliyoshuhudiwa wakati wa janga la UVIKO-19, ambapo wakati huo kulikuwa na hatari kubwa ya kugusa vitu mbalimbali. Pia wanasema walishinikizwa na uimarishaji jumla wa usafi na kupunguza harakati za binadamu kugusa uchafu.
“Wakati wa virusi vya corona tuliona tutengeneze hili pipa ili liwasaidie watu kutupa takataka bila kugusa uchafu. Tuliona virusi na uchafu ni vingi kwenye mazingira. Mtu anapoisogelea hii “ultra sonic sensa” ya hili pipa linajifungua lenyewe. Halafu utatupa takataka yako, baada ya sekunde 3 litajifunga tena lenyewe,” alisema Keicy.
Kwa upande wake Shanice anasema walizungumza na mwalimu wao na kumuuliza njia za kujaribu kupunguza idadi ya maambukizi ya Corona wakati huo ndipo wakabuni pipa hili la taka.
” Tulitaka kupunguza kiwango cha watu kugusa uchafu kwa haraka bila kushika uchafu, kwa sababu watu wanashika uchafu ndivyo wanapata magonjwa. Tukaona namna tunavyoweza kutengeneza kitu ambacho mtu hashiki kwa mkono, ” alieleza Shanice.
Mabinti hao ni fahari kwa walimu na wazazi
Mwalimu mwelekezi Hillary Omondi Otieno wa somo la tarakilishi na hesabu anasema, kando na mifumo hiyo ya nishati, vile vile pipa hili linaweza kutumia nguvu za nishati ya jua.
” Linaweza kutumia umeme wa jua, sio lazima litumie tu umeme wa kawaida, pili, hili pipa linaweza kutumiwa kila mahali, unaweza kuliweka kwenye ofisi. Na pipa la aina hii linahitajika sana hospitali kwa sababu kuna changamoto. Hili pipa tunaweza kulifunga kama vile umeona tumelifunga hivyo kila kitu ili mvua isiweze kunyeshea hizo taka za ndani, ” alisema mwalimu Hillary Otieno.
Kwa kuunganisha vifaa mbalimbali ili kuunda kifaa hiki, mwanzoni walitumia mkaa wenye volti 12 na ili kuongeza nguvu zaidi, wakaimarisha mfumo huu kwa kutumia chaji ya umeme ili kuzingatia suala zima la mazingira . Kwenye harakati za ubunifu wanafunzi hawa wanasema haikuwa rahisi maana ilihitaji maarifa mengi yanayojumuisha mfumo wa maandalizi ya programu maarufu kama “coding” ambayo inahusisha kuandaa utaratibu wa mawazo ya ubunifu na kuyaweka katika kifaa mahsusi.
Mfano, ikiwa unataka mashine inayojifungua, unatakiwa kuweka ufafanuzi huo katika mfumo wa coding. Walifeli mara kadhaa, ila mwalimu aliwaelekeza katika harakati hizi na kuendelea kuwatia moyo.
” Tulikuwa wanane tulipoanza, tukamaliza wawili. Nilijiambia kwamba hili jambo linaweza kunifanya niwe mtu bora maishani. Tuliona pia tutafute njia za kuwafurahisha wazazi wetu, ” walisema Shanice na Keicy.
Bila shaka ni fahari kubwa kwa mzazi pindi mtoto anapofanya jambo kubwa katika jamii, Roseline Awuor mama yake Shanice Achieng pamoja na Eunice Odera, shangazi yake Kaicy, wanawahimiza wazazi kuwa mstari wa mbele katika kutambua na kulea vipaji vya watoto wao sawia na kuwaunga mkono kwenye harakati zao.
” Wazazi tuwape watoto nafasi kwa sasabu inaweza kuwa na manufaa kwenye maisha yao. Tulionyeshwa na mwalimu, tukaitwa kama wazazi tukajionea jinsi teknolojia ya wakati huu inaenda mbali, ” walisema wazazi hao.
Uvumbuzi wa wanafunzi hao wawili kutoka Kisumu-Kenya waliobuni pipa la kisasa linalojifungua na kurahisisha utupaji taka ni wa kupongezwa na unatoa matumaini kwa vijana wa kiafrika kuendelea kupata ujuzi zaidi ili na wao wawe mstari wa mbele katika ubunifu wa vitu mbalimbali.