
Msemaji wa ofisi hiyo ya Umoja wa Mataifa Thameen Al-Keetan, amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kwamba miezi kumi na moja tangu kuanguka kwa serikali ya zamani nchini Syria, wanaendelea kupokea ripoti zinazotia wasiwasi kuhusu watu kutekwa nyara na kupotezwa kwa nguvu.
Ofisi hiyo imerekodi angalau watu 97 ambao wametekwa nyara au kutoweka tangu Januari mwaka huu, na kusema ni vigumu kupata takwimu sahihi.
Hali ya usalama Syria yafanya kuwe vigumu kuwatafuta watu waliopotea
Pia imesema hali tete ya usalama nchini Syria, kufuatia kuzuka kwa ghasia katika eneo la pwani na mji wa kusini wa Sweida, imefanya kuwa vigumu kuwapata ama kuwafuatilia watu waliopotea kwasababu baadhi wanaogopa kutoa maelezo.
Al-Keetan ameongeza kuwa baadhi ya watu walikabiliwa na vitisho kwa kuzungumza na Umoja wa Mataifa.