Iran imekadhibisha vikali madai yaliyotolewa na Marekani na Israel kwamba Jamhuri ya Kiislamu ilikuwa na mipango ya kumuua balozi wa Israeli nchini Mexico, ikiyataja madai hayo kuwa ni “uongo mkubwa.”

Katika ujumbe wake kwenye jukwaa la X jana Ijumaa, ubalozi wa Iran nchini Mexico, uliyataja madai hayo kuwa ni uzushi wa kipropaganda unaolenga kuharibu uhusiano wa kirafiki na wa kihistoria kati ya Tehran na Mexico.

“Tuhuma kuhusu eti jaribio la Iran la kumuua balozi wa utawala wa Israel huko Mexico ni uzushi wa kivyombo vya habari na uongo mkubwa, ambao lengo lake ni kuharibu uhusiano wa kirafiki na wa kihistoria kati ya nchi zote mbili (Mexico na Iran); tunaupinga kabisa,” umesema ujumbe wa ubalozi wa Iran huko Mexico kwenye mtandao wa kijamii wa X.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa: “Hii si mara yao ya kwanza kujaribu kuharibu uhusiano wa Iran na nchi zingine kupitia habari bandia.” 

Wakati huo huo, serikali ya Mexico imetangaza kwamba “haina taarifa yoyote kuhusu shambulio linalodaiwa kumlenga balozi wa Israel nchini Mexico.”

Taarifa ya pamoja kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Wizara ya Usalama wa Ndani ya Mexico imesema hakuna ripoti za madai ya shambulio dhidi ya balozi wa Israel nchini, na kwamba Mexico haikupokea taarifa zozote zinazothibitisha madai ya njama dhidi ya balozi huyo.

Hii si mara ya kwanza Iran kutuhumiwa kupanga mauaji dhidi ya wanadiplomasia au wapinzani nje ya nchi bila ushahidi wowote. Kinyume chake, Israel na Marekani zina rekodi ndefu ya kuwalenga maafisa wa Iran katika operesheni zinazofanywa katika nchi za nje.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *