
Dar es Salaam. Kizazi cha sasa hakina muda wa kusubiri taarifa kwenye TV. Kila kitu kiko mkononi. Kwenye X (Twitter), Instagram, Tiktok au Youtube, ndio huko ndiko habari, siasa, hata drama za kitaifa zinapochomoka. Achana na grupu za wasapu.
Na ukweli ni kwamba, mitandao imekuwa uwanja wa kivita wa karne hii. Lakini vita hii si ya risasi ni ya likes, captions, hashtags na tweets zenye sumu kali. Kimsingi haya mambo yapo dunia ya tatu ya wazee wa mapokeo
Kuna wapiganaji wa kidigitali, ndo ‘mashujaa’ wa mitandaoni. Wanaojitangaza kama watetezi wa haki, wazalendo, wachambuzi au wenye akili zaidi. Lakini ndani ya pazia, kila mmoja ana “ajenda” yake.
Mwingine anapigania siasa kweli, mwingine anatafuta followers tu, na mwingine ndo kazini kwake, anapiga kelele kwa malipo. Kuna wale bendera fuata upepo ambao huwa mashabiki na wenye timu zisizo na makocha.
Sasa hivi, siasa na mitandao zimeoana. Kila chama, na kila mwanasiasa, kila taasisi inatafuta “mshauri wa digital.” Wanataka mtu anayejua kutrendi, ambaye anayeweza kubadilisha hisia za watu kwa tweet moja tu.
Mitandao imegeuka kama jukwaa la kampeni zisizo rasmi. Huko ndikoo hoja, propaganda, hata majibu ya serikali hupeperushwa, mmoja akishambulia, mwingine anajibu, na wafuasi wakishangilia kama mechi ya Simba na Yanga.
Ushawishi ni mkwanja, usipige kelele bure! Katika mchezo huu wa kidigitali, pesa inazunguka. Kuna wanasiasa wanaowalipa influencers ili wapige kelele kwa niaba yao. Tena hawa ndiyo wengi sana.
Kuna mashirika ya kimataifa yanayolipa “campaigns” za haki za binadamu, mazingira au demokrasia. Kuna mabizinesi man na mabizinesi woman hata wamisionari wa kizazi hiki, Papa John Paul 11 alikiita kizazi cha CNN.
Kuna wafanyabiashara wanataka wapinzani wao kibiashara labda wachafuliwe kidogo mitandaoni. Siyo kwa sababu ya uhalali, bali kwa sababu ya ushindani. Wote hawa hutumia pesa mitandaoni huko, wenye ushawishi wanapiga pesa.
Kwa hiyo, usishangae kuona post moja tu imevuma sana, nyuma yake kuna mkataba, invoice, au mobile money alert ya kufa mtu! Usiwe pimbi kushabikia kibwege kwa likes na coments za kindezi. Wenzako wana make money then wanatumia kwa akaunti.
Na wale mashabiki wanakuwa ndo silaha kubwa. Kile ambacho zamani kilikuwa ni wafuasi wa vyama, kimehamia mtandaoni. Wafuasi mitandaoni wanapigana kama askari, wanashambulia, wanatetea, wanatukana na hata kujenga hoja.
Lakini mara nyingi, hawajui kwamba wanatumiwa kwenye vita vya ajenda. Wao wanakuwa “keyboard warriors” bila kujua kwamba kila tweet yao ni risasi ya mtu mwingine. Na hawa ndiyo wengi na washamba wakubwa wa mitandao.
Mashabiki wengi wanadhani wanatetea nchi au haki. Kumbe pale wanasaidia kutengeneza engagement ya mtu. Anayelipwa kwa kila trending topic. Ni kama drafti wewe unacheza, lakini pesa inaenda kwa mwenye ubao!
Wapya wanaoibuka day to day. Ni kizazi kipya cha influencers wa kisiasa. Hawa siyo wanasiasa rasmi, lakini wana sauti kubwa kuliko wabunge wengine. Wana mamilioni ya wafuasi wanaowatii, kusikiliza na kufuata elekezo.
Kuna wanaochambua siasa kwa utani, wengine kwa hasira hasira. Na wengine kwa ucheshi, lakini mwisho wa siku, wote wana impact. Mitandao ni chombo cha kuunganishwa, lakini imekua kama meza ya mikutano ya kisiasa.
Hata mataifa makubwa sasa yanawekeza kwenye “digital intelligence.” Afrika mashariki haiko nyuma, kila nchi ina kundi lake la vijana wanaotumia hiyo mitandao kama “ngome ya kisiasa.” Kuanzia nakuru mpaka mbinga wapo.
Nani anamiliki ashawishi? Ujue. Ushawishi ni nguvu. Kama ilivyo nguvu yoyote, ikitumika vibaya inaweza kuharibu. Leo hii, mtu mmoja anaweza kupindua maoni ya maelfu kupitia post moja tu.
Anaweza kuharibu sifa ya mtu, biashara, au hata kuanzisha hofu ndani ya jamii.
Lakini pia, mtu huyo huyo anaweza kutumia nguvu hiyo kuelimisha, kuhamasisha, na kuleta mabadiliko. Hapo ndipo siri ya ushawishi ilipo, ni silaha, na silaha haipendelei mtu. Awaye yeyote inaweza kutumika kutoa uhai wake.
Kwa hiyo, vijana wa sasa wanapaswa kuwa makini.
Mitandao ni fursa kubwa, lakini ni mtego mkubwa pia. Unaweza kujenga jina lako au kuliharibu kwa post moja tu. Na kumbuka kwenye dunia ya kidigitali, delete haimaanishi imesahaulika.
Ni sauti rasmi ya kizazi kipya hiki. Ndio, mitandao imegeuka bunge la vijana. Ni sehemu ya kueleza maoni, kulalamika, kuelimishana na kuishi maisha ya kisasa. Lakini kama tutaitumia vibaya, inaweza kuwa moto unaochoma kila kitu.
Tufanye mitandao kuwa jukwaa la ubunifu, si majukwaa ya malipo ya ajenda. Kwa sababu followers wako wanakuamini, basi una deni la kusema ukweli, si kuuzia watu chuki, uhasama na lolote baya kwa ubaya.
Mitandao ni sumu kama sumu zingine. Mitandao ni nguvu, ushawishi ni pesa, lakini busara ndiyo mfalme. Kama unataka kuwa na impact ya kudumu, tafuta heshima na siyo trending tu!