Dar es Salaam. Simba imekwea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya JKT Tanzania.

Mabao ya ushindi ya Simba yote yamepachikwa katika kipindi cha pili na Wilson Nangu na Jonathan Sowah huku lile la JKT Tanzania likipachikwa na Edward Songo.

Ushindi wa Simba katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni Dar es Salaam umeifanya ifikishe pointi tisa ambazo zimeipandisha kileleni mwa msimamo wa ligi.

Kwa kupoteza mechi hiyo, JKT Tanzania imeporomoka hadi katika nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi kutoka nafasi ya tano iliyokuwepo awali.

Hata hivyo, Simba inaweza kukaa kileleni kwa muda kwani timu kama Yanga ikiibuka na ushindi dhidi ya KMC kesho, itapanda kileleni ikifikisha pointi 10.

Katika mchezo mwingine wa Ligi hiyo uliochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Pamba Jiji FC imetoka sare ya bao 1-1 na Singida Black Stars.

Singida ilikuwa ya kwanza kupata bao mnamo dakika ya 31 likifungwa na Clatous Chama kwa faulo ya moja kwa moja ilyozama nyavuni na kumshinda kipa wa Pamba Jiji, Yona Amosi.

Pamba Jiji wamesawazisha bao hilo kipindi cha pili katika dakika ya 51 likifungwa na Kelvin Nashon kwa shuti kali ambalo limemshinda kipa baada ya kuumalizia mpira uliokuwa unazagaa eneo la hatari baada ya kuwababatiza mabeki.

Baada ya matokeo hayo, Pamba Jiji imefikisha alama tisa na kuongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara, ikiwa imecheza michezo sita ikishinda miwili, sare tatu na kupoteza moja, huku Singida ikiwa katika nafasi ya nane na alama zake Saba baada ya michezo mitatu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *