
Jeshi la Somalia jana Jumapili lilifanya oparesheni kadhaa katika majimbo ya Bakool na Bay na kuuwa wanachama wa ngazi ya juu wa kundi la kigaidi la al Shabaab.
Wizara ya Ulinzi ya Somalia imeeleza kuwa askari jeshi wa nchi hiyo wamemuuwa Abdi Mohamed Nur anayefahamika pia kwa jina la Goofoow mwanachama wa ngazi ya juu wa kundi hilo la kigaidi ambaye amehusika na mashambulizi kadhaa dhidi ya raia huko Somalia.
Abdi Mohamed Nur ameuawa katika kijiji cha mkakakati cha Abal yapata umbali wa kilomita 21 kusini mwa Hudur, makao makuu ya jimbo la Bakool linalopatikana kusini magharibi mwa Somalia.
Katika oparesheni hizo dhidi ya al Shabaab, jeshi la Somalia lilinasa pia silaha kadhaa na hati kuhusu njama zilizokuwa zimeratibiwa na al Shabaabili kuvuruga usalama na amani huko Somalia.
Jeshi la Somalia pia jana liliwauwa watendaji wakuu wa kundi la kigaidi la al Shabaab kwa majina ya Yahye anayejulikana pia kwa jina la Abu Khalid mratibu mkuu wa mashambulizi ya kigaidi, na Sharif Amir .
Taarifa ya Wizara ya Uinzi ya Somalia imeeleza kuwa, Amir alijeruhiwa katika oparesheni ya Jumapili na aliaga dunia baadaye kutokana na majeraha makubwa aliyopata wakati wa shambulizi.
“Jeshi la Somalia litaendelea kufanya oparesheni dhidi ya al Shabaab na hakuna sehemu salama ya kujificha magaidi wa kundi hilo,” imeeleza taarifa ya Wizara ya Ulinzi ya Somalia.
Wizara ya Ulinzi ya Somalia imesisitiza kuwa: Operesheni zinazoendelea kufanywa ili kudumisha amani katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika zitaimarishwa “hadi kila kona ya Somalia itakapoondokana na tishio la ugaidi,”
Jeshi la Somalia jana Jumapili zilitekeleza operesheni hizo dhidi ya magaidi wa kundi la al Shabaab ikiwa zimepita siku kadhaa baada ya Somalia kutangaza kutekeleza kwa usahihi mashambulizi 220 ya anga dhidi ya al Shabaab tangu Februari mwaka huu. Jumla ya magaidi 868 wa al Shabaab wameuawa katika oparesheni hizo.