Rais wa Marekani alitangaza kuwa, hakuna maafisa wa Marekani watakaohudhuria mkutano wa kila mwaka wa Kundi la G20 huko Johannesburg, Afrika Kusini.
Uamuzi huo, ulioelezwa kuwa ni kususia kabisa, sio tu kwamba ulighairi kuhudhuria Makamu wa Rais James David Vance, lakini pia uliiondoa Marekani kwenye mojawapo ya mikutano muhimu zaidi ya kiuchumi duniani.
Rais wa Marekani Donald Trump aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa Truth Social: “Ni fedheha kubwa kwamba mkutano wa G20 unafanyika Afrika Kusini. Waafrikana (wajukuu wa wahamiaji wa Uholanzi, Wafaransa na Wajerumani) wanauawa na kuchinjwa na ardhi na mashamba yao kuchukuliwa kinyume cha sheria, hivyo hatashiriki mkutano huo.”
Matamshi haya, yanayotokana na madai yaliyokanushwa ya “mauaji ya halaiki ya wazungu” nchini Afrika Kusini, ni kifuniko tu cha nia halisi ya Trump ya kuiadhibu Afrika Kusini kwa kuishitaki Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kwa mauaji ya kimbari huko Gaza.
Ili kuelewa uamuzi huu, ni muhimu kuangalia muktadha mpana. Trump amekuwa akiendesha kampeni ya kimfumo dhidi ya Afrika Kusini tangu arejee Ikulu ya Marekani Januari 2025. Mnamo Februari mwaka huu, alitoa amri ya utendaji ya kukata misaada yote ya Marekani kwa Pretoria na kukubali wakulima 59 wa Kiafrikana nchini Marekani kama “wakimbizi.”

Hatua hizi, ambazo zimekataliwa na mahakama za Afrika Kusini na mashirika ya haki za binadamu kama vile Amnesty International, zinatokana na takwimu bandia na video zilizotiwa mkono (kama vile picha kutoka Kongo zilizowasilishwa kama ushahidi wa mauaji ya wakulima wa Afrika Kusini).
Takwimu rasmi zinaonyesha kwamba, mauaji ya wakulima wa kizungu yanachangia asilimia 0.4 pekee ya mauaji yote ya kila mwaka (zaidi ya kesi 27,000) na kwamba hakuna unyakuzi uliofanywa na serikali bila ya fidia ya kifedha.
Hata hivyo, Trump anatumia simulizi hii kuhamasisha wapiga kura wake wa mrengo wa kulia, ambao wanavutiwa na nadharia za njama za ubaguzi wa rangi. Lakini sababu halisi ya vikwazo hivi ni sera ya kigeni ya Afrika Kusini.
Mnamo Desemba 2023, Afrika Kusini iliwasilisha malalamiko ya kihistoria dhidi ya Israel kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICJ), ikitangaza kwamba operesheni za kijeshi za Israel huko Gaza, ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya mabomu dhidi ya raia, mzingiro kamili na matamshi ya maafisa wa Israel kuhusu “maangamizi ya Gaza,” yanajumuisha mauaji ya kimbari chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa 1948.
Kesi hiyo, iliyotokana na uzoefu wa Afrika Kusini na ubaguzi wa rangi, iliwasilisha ushahidi kama vile kuuawa shahidi kwa zaidi ya Wapalestina 48,000 (ikiwa ni pamoja na watoto 20,000) na uharibifu wa miundombinu ya Gaza.
ICJ iliamua mnamo Januari 2024 kwamba madai ya mauaji ya halaiki “yanapitiwa upya” na ilitoa maagizo ya muda: Israel lazima ikomeshe operesheni za kijeshi huko Rafah, kuzuia mauaji ya halaiki, na kuruhusu msaada wa kibinadamu kuingia huko. Kufikia sasa, zaidi ya nchi 14, zikiwemo Uturuki, Uhispania, Colombia na Bolivia, zimejiunga na kesi hiyo kama wasuluhishi, na Israel inashutumiwa kwa kukosa kufuata maamuzi.
Trump, ambaye anaiona Israel kama mshirika wa karibu wa Marekani, ameitaja kesi hiyo “ya uchokozi” na “inayopinga Marekani.” Katika agizo kuu la Februari 2025, aliashiria kwa uwazi kesi ya ICJ na kuichanganya na madai ya ndani ya Afrika Kusini.

Wachambuzi kama vile Saul Dubow wa Chuo Kikuu cha Cambridge wanaelezea njia hii kama “Ndoto ya Trump” ili kupotosha umakini kutoka kwa mauaji ya kimbari huko Gaza. “Tunawezaje kwenda katika mkutano wa G20 nchini Afrika Kusini wakati unyakuzi wa ardhi na mauaji ya halaiki ndio mada kuu ya majadiliano?” Trump alisema katika hotuba ya Aprili 2025 huko Miami.
Kususia mkutano wa kilele wa G20, ambao Afrika Kusini ni mwenyekiti wake kuanzia Desemba 2024, ni sehemu ya mkakati huu wa mashinikizo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio hapo awali alisusia mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa G20 kwa kuangazia “anuwai, usawa na uendelevu” mada ambazo Trump anaziita za mrengo wa kushoto.
Hata hivyo radiamali ya Afrika Kusini imekuwa kali. Rais Cyril Ramaphosa ameyataja madai ya Trump kuwa “yanaeneza uwongo” na kusisitiza kwamba Waafrika Kusini weupe wanafurahia maisha ya juu kuliko weusi walio wengi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini Ronald Lamola pia alisema siku chache zilizopita: “Hakuna nafasi ya kurudi nyuma kuhusiana na kesi dhidi ya Israel. Kusimama kwenye kanuni wakati mwingine kuna gharama, lakini ni muhimu kwa utawala wa sheria za kimataifa.”
Hatua ya Marekani ya kususia mkutano wa kilele wa G20 nchini Afrika Kusini sio tu itazorotesha uhusiano baina ya nchi hizo mbili bali pia itakuwa na athari za kimataifa. G20, ambayo inawakilisha asilimia 85 ya uchumi wa dunia, inaweza kuelekea kwenye miungano mbadala kama vile BRICS (ambayo Afrika Kusini ni mwanachama) bila Marekani, tukio ambalo litaiweka Marekani chini ya mashinikizo makubwa zaidi.