KOCHA wa Mbeya City, Malale Hamsini amesema licha ya kazi ya benchi la ufundi la kutengeneza timu bora na ya ushindani, ila kwa sasa ni muda wa wachezaji wa kikosi hicho kujifanyia pia tathimini kutokana na makosa ya kujirudia wanayofanya.

Akizungumza na Mwanaspoti, Malale amesema hadi sasa hawako sehemu mbaya sana ingawa walistahili zaidi ya hapo walipo, japo changamoto kubwa ni makosa ya mara kwa mara na kukosa umakini katika eneo la kujilinda na lile la ushambuliaji.

“Mechi mbili zilizopita tulistahili kupata pointi tatu au hata nne kati ya sita, lakini haikuwa hivyo, tunapoteza nafasi za kufunga kwa sababu ya kukosa umakini, ni jukumu letu benchi la ufundi na wachezaji kulifanyia kazi,” amesema Malale.

Kocha huyo wa zamani wa maafande wa Polisi Tanzania, amesema moja ya jambo analoliona ni kila mchezaji kufanya uamuzi wa haraka hata kama hayuko sehemu nzuri ya kufanya hivyo, kitu ambacho anaendelea kupambana nacho kabla ya Ligi haijarejea.

Timu hiyo iliyopanda Ligi Kuu msimu huu, imecheza mechi sita na kati ya hizo imeshinda mbili, ikitoka sare mbili na kupoteza pia mbili, ikiongoza na pointi zake nane.

Malale aliyejiunga na timu hiyo Machi 31, 2025, akichukua nafasi ya Salum Mayanga aliyejiunga na Mashujaa, amekipandisha kikosi hicho Ligi Kuu Bara, ikiwa ni mara ya pili baada ya kufanya hivyo pia, akiwa na JKT Tanzania msimu wa 2022-2023.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *