Bidhaa za wajasiriamali wa Tanzania wanaoshiriki Maonesho ya 25 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) yajulikanayo kwa jina maarufu la ‘Nguvu Kazi’ au ‘Jua Kali’ zimeendelea kufanya vizuri kwenye maøensho hayo yanayoendelea jijini Nairobi, Kenya.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wajasiriamali hao wamesema Serikali imewasaidia kuzifihkisha bidhaa hizo kwenye soko hilo kwa kugharamia usafiri pamoja na mizigo jambo ambalo limeongeza ari na hamasa ya kushiriki kwa wingi katika maonesho hayo.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati katika Jumuiya ya Afrika Mashariki upande wa Tanzania (CISO–Tanzania), Josephat Rweyemamu, amesema serikali imeendelea kuratibu ushiriki wa wajasiriamali hao na kuwawezesha kutangaza bidhaa na huduma zao nje ya mipaka ya Tanzania hali inayowaongezea soko la bidhaa zao na kuanzisha ushirikiano na wajasiriamali wa mataifa mengine.
“Tunaishukuru sana serikali kwa kutuwezesha kwa kila namna kuweza kufika Nairobi na kutumia hii fursa ya kipekee kwetu kufanya na kukuza biashara zetu na kujifunza kutoka kwa wajasiriamali wa nchi nyingine,” amesema mmoja wa washiriki.
Maonesho ya 25 ya wajasiriamali wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yameambatana na kaulimbiu “Miaka 25 ya Ujumuishaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki: Kuendeleza Ubunifu na Minyororo ya Thamani ya Kikanda kwa Biashara Ndogo na za Kati Shindani kuelekea Maendeleo Endelevu” na yanatarajiwa kutamatika Novemba 16 mwaka huu.
Imeandaliwa na @moseskwindi