
BAADA ya upangaji wa makundi ya road to BAL Elite 16 kufanyika, wababe wa kikapu nchini, Dar City imeshauriwa kusajili nyota wengine wapya wenye uzoefu ili waisaidie kutimiza lengo la kuleta ubingwa Afrika hapa nchini.
Mashindano hayo ya hatua ya pili yanalenga kuiwezesha timu hiyo kufuzu Ligi ya Kikapu Afrika (BAL), ambapo imepangwa
katika kundi B na timu za Brave Hearts BC ya Malawi, Matero Magic (Zambia) na Ferrviario Da Beira ya Msumbiji.
Akizungumza na Mwanaspoti, kocha mkogwe nchini, Denis Lipiki ameutaka uongozi wa Dar City kusajili wachezaji wenye uzoefu mkubwa wa mashindano ya Afrika. Mashindano hayo yanaanza Novemba 18-23, mwaka huu katika Uwanja wa Ndani wa Kasarani, Kenya.
Lipiki ameliambia Mwanaspoti kuwa licha ya timu hiyo kuwa na mastaa wenye viwango bora, lakini anaamini wakipatikana wengine wa kuongezea wenye uzoefu na mashindano hayo watasaidia kuiwezesha kufanya vizuri zaidi ili icheze fainali ya mashindano ya ubingwa wa Afrika mwakani na hatimaye kuuvuta ubingwa hapa nchini.
Kocha huyo anayefundisha katika kituo cha Ukonga Academy, Dar es Salaam aliutaka uongozi kusaka mechi moja ya kimataifa ya kirafiki ili kuwaweka fiti zaidi mastaa waliopo kwa ajili ya michuano hiyo.
“Dar City ikifanya hivyo nina uhakika itafika fainali ya mashindano hayo ya BAL bila matatizo yoyote,” alisema Lipiki.
Kocha huyo alisema kwa kariba ya mashindano hayo ni suala gumu kupenya ikiwa timu haitakuwa na maandalizi mazuri yanayonogeshwa na mastaa wenye ubora wa kimataifa.
Timu nane zimefuzu kucheza hatua hiyo kuelekea kwenye fainali, ambapo kundi A la mashindano litakuwa na timu za Nairobi Thunder (Kenya), Johannburg Giants (Afrika Kusini) na Namuwongo Blazers (Uganda).
Akizungumzia suala la kanuni na utaratibu wa mashindano hayo, meneja wa Dar City, Simon Joe amesema timu mbilimbili za juu kutoka kundi A na B zitacheza zenyewe na mbili zitakazofanya vizuri zitatinga hatua ya robo fainali ambapo zitaungana na sita zingine zilizofanya vizuri katika maeneo mengine.
Dar City na Namuwongo Blazers zilifuzu kucheza hatua ya road to BAL Elite 16 baada ya kufanya vizuri katika mashindano yaliyofanyika katika Uwanja wa Shule ya Kimataifa Tanganyika (IST) iliyopo Masaki, Dar es Salaam, ambapo Dar City iliishinda Djabar ya Comoro kwa pointi 102-50 na Namuwongo Blazers 83-70.
Namuwongo Blazers ilifuzu baada ya kuishinda Djabar kwa pointi 132-58 na mchezo wa pili ilifungwa na Dar City kwa pointi 83-70. Mashindano hayo ya kundi D yalishirikisha Dar City, Namuwongo Blazers na Djabar.