Ripoti mpya ya pamoja ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) la na Mpango wa Chakula Duniani (WFP) iliyotolewa leo Jumatano zimetahadharisha kuwa, hali ya ukosefu wa usalama wa chakula inazidi kuwa mbaya katika maeneo 16 yenye janga la njaa duniani, huku mamilioni ya watu wakiwa katika hatari ya kupatwa na janga hilo katika kipindi cha kati ya Novemba 2025 na Mei 2026.

Kwa mujibu wa ripoti kuhusuu Maeneo yenye Njaa, migogoro na machafuko ndivyo vichocheo vikuu vya baa la njaa katika maeneo 14 yaliyoathiriwa.

Nchi na maeneo yenye kutia wasiwasi mkubwa ni pamoja na Haiti, Mali, Palestina, Sudan Kusini, Sudan, na Yemen, ambapo watu wa maeneo hayo wanakabiliwa na hatari kubwa ya njaa. Afghanistan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Myanmar, Nigeria, Somalia, na Syria zimeorodheshwa kuwa ni zenye kuzusha “wasiwasi mkubwa sana,” huku wakimbizi wa Burkina Faso, Chad, Kenya, na wa Rohingya walioko nchini Bangladesh nao pia wakiwa wanakabiliwa na hali mbaya.

Ripoti hiyo imeonya kwamba “muda unaisha haraka kwa ajili ya kuepuka baa la njaa linaloenea” kwani ufadhili wa misaada ya kibinadamu unabaki kuwa mdogo sana. Kufikia mwishoni mwa Oktoba, ni dola bilioni 10.5 pekee kati ya dola bilioni 29 zinazohitajika kuwasaidia wale walio katika hatari kubwa zilikuwa zimepokelewa, na kulazimisha mashirika kupunguza mgao wa chakula na kusimamisha programu za lishe na utoaji chakula mashuleni.

Mkurugenzi Mkuu wa FAO QU Dongyu amesema: “mifumo ya tahadhari za mapema duniani inafanya kazi – hii ni muhimu kwa hatua za mapema. Lazima tuache kukabiliana na migogoro, tuizuie. Kuwekeza katika riziki, ustahimilivu na ulinzi wa kijamii kabla ya kilele cha njaa kutaokoa maisha na rasilimali. Kuzuia njaa si wajibu wa kimaadili tu, ni uwekezaji mzuri katika amani na utulivu wa muda mrefu. Amani ni sharti la usalama wa chakula na haki ya chakula ni haki ya msingi ya binadamu.”

“Tuko kwenye ukingo wa janga la njaa linaloweza kuzuilika kabisa ambalo linatishia njaa iliyoenea katika nchi nyingi,” ameeleza pia Mkurugenzi Mtendaji wa WFP Cindy McCain.

FAO na WFP zimetoa wito wa ufadhili wa haraka, utashi wa kisiasa, na ufikiaji wa kutoa misaada ya kibinadamu usio na vizuizi ili kuzuia njaa kabla ya kuchelewa…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *