Osama Hamdan, kiongozi mwandamizi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS, amesisitiza kwamba, silaha za Muqawama ni suala lisiloweza kujadiliwa kabla ya kuundwa nchi dola ya Palestina na akabainisha kuwa, lengo la kisiasa la Muqawama litabaki kuwa ni kuikomboa ardhi, kuundwa nchi huru ya Palestina ambayo mji mkuu wake ni Baitul-Muqaddas na kuwepo hakikisho la kurejea wakimbizi.

Hamdan ameeleza kwamba, makubaliano ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Ghaza ni ya kuhitimisha uchokozi wa adui na kuanza uchukuaji wa hatua za kisiasa na kitaifa za Palestina.

Ameongeza kuwa, harakati ya Hamas imeamiliana na makubaliano ya kusitisha mapigano kwa sura ya kubeba masuulia na kuwajibika kitaifa na kwa kuzingatia muelekeo wa wazi wa kulinda misingi na haki za Palestina, na kwamba makubaliano hayo ni tofauti na makubaliano yaliyopita, kwa sababu yameeleza bayana kuhusu kusimamishwa vita kikamilifu na yanaashiria utangulizi wa kisiasa kuelekea kwenye kutambuliwa haki ya Wapalestina ya kuwa na nchi yao huru.

Kiongozi huyo mwandamizi wa Hamas ameendelea kueleza kuwa, mazungumzo yaliyopelekea kufikiwa makubaliano ya kusitisha vita yalilenga katika hatua ya kwanza kusimamisha vita hivyo, kubadilishana mateka, kuingizwa misaada ya kibinadamu Ghaza, na kuondoka vikosi vya utawala ghasibu wa kizayuni katika eneo hilo.

Kuhusu uendeshaji wa Ukanda wa Ghaza baada ya vita, Hamdan amesema, makubaliano ya awali yalihusu kuundwa kamati ya uendeshaji wa masuala ya Ghaza katika kipindi cha mpito, lakini maelezo zaidi kuhusu utendaji kazi wa kamati hiyo na mamlaka itakayokuwa nayo lingali ni suala la kujadiliwa kitaifa miongoni na makundi ya Palestina.

Kadhalika, kiongozi huyo mwandamizi wa Hamas amesisitizia haki ya Muqawama ambayo ni haki thabiti, yenye uhalali wa kisheria na isiyoweza kulegezewa msimamo, inayohusiana na kabla ya kuasisiwa nchi dola ya Palestina itakayokuwa na uwezo wa kuwalinda watu wake na ardhi yake; na akabainisha kwamba, mazungumzo yoyote kuhusu silaha za Muqawama yataahirishwa hadi baada ya kuundwa nchi huru ya Palestina, na kwamba tajiriba ya huko nyuma inaonyesha kuwa, muelekeo wowote unaong’ang’ania suala la upokonyaji silaha au kulegeza msimamo kuhusu haki za taifa la Palestina umefeli na kugonga mwamba…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *