
Ongezeko la bei za baadhi ya bidhaa za kimsingi nchini Marekani limeilazimisha serikali kujizuia kutoza ushuru wa ziada kwa uagizaji wa baadhi ya bidhaa kutoka Amerika Kusini.
Jarida la Marekani Politico limeripoti kuwa: Chanzo kimoja katika Ikulu ya Marekani White House kimetangaza kusainiwa mikataba mipya ya kibiashara na nchi nne za Amerika Kusini na Kati ambayo itapelekea kupunguzwa kwa ushuru wa forodha kwa baadhi ya bidhaa kama vile kahawa, ndizi na nyama ya ng’ombe.
Jarida la Politico limeongeza kuwa: Kwa mujibu wa taarifa za afisa mmoja mwandamizi wa utawala wa Trump, makubaliano na nchi hizi nne yatakamilika ndani ya wiki mbili zijazo, na kuna uwezekano wa kufikia makubaliano zaidi ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.
Kwa mujibu wa Politico, utawala wa Trump unatazamiwa kusaini mikataba mipya ya kibiashara na Argentina, Guatemala, El Salvador na Ecuador ambayo itapunguza ushuru wa kuagiza baadhi ya bidhaa, ikiwa ni pamoja na nyama ya ng’ombe ya Argentina, kahawa na ndizi.
Washauri wa masuala ya kiuchumi wa Trump wamesema kupunguza ushuru ni sehemu ya juhudi za serikali za kupunguza bei, na kwamba bei za bidhaa kama vile kahawa na ndizi zinaweza kushuka.
Indhari na radiamali zimekuwa zikitolewa ndani ya Marekani na kimataifa kutokana na kuendelea vita vya ushuru vya Rais Donald Trump na madai yake katika uwanja huo.
Tangu aingie madarakani katika muhula wake wa pili, Rais wa Marekani alianzisha wimbi la vita vya ushuru hususan kwa mataifa ambayo yanaonekana kuwa washindani au wapinzani wa dola hilo la kibeberu hatua ambazo sasa zimekuwa na taathira hasi nchini Marekani