
Waziri wa Turathi za Utamaduni na Utalii wa Iran ametangaza kuongezeka kwa idadi ya watalii wa kigeni wanaoingia na kutembelea Iran.
Seyyed Reza Salehi Amiri, Waziri wa Utalii wa Iran amesema katika mahojiano na Shirika la Habari la Fars: “Mwezi wa Aprili na Mei mwaka huu, kulirekodiwa ongezeko la watalii kwa zaidi ya 30%, na tangu Septemba na Oktoba, kumekuwa na mwenendo wa kupanda ongezeko la watalii wa kigeni hapa nchini.
Kwa mujibu wa Pars Today amesema kuwa, watalii 3,000,550 waliingia Iran katika nusu ya kwanza ya mwaka huu na kutabiri kuwa hadi mwisho wa mwaka huu, idadi ya watalii wanaoingia Iran itafikia zaidi ya milioni 7.
Salehi Amiri alisisitiza: Iran, ikiwa na turathi tajiri za kiutamaduni, mandhari tofauti na athari za kipekee za kihistoria, ni moja ya vivutio vikubwa zaidi vya watalii ulimwenguni.
Waziri wa Utalii wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia ameashiria kusajiliwa kwa vijiji vitatu vya Iran katika orodha ya Shirika la Utalii Duniani na kuongeza kuwa: “Mwaka 2025, Iran ilitambulisha vijiji vinane, ambapo Hasanlu, Fahraj na Shafiabad vilifanikiwa kusajiliwa katika Shirika la Utalii Duniani.”
Itakumbukwa kuwa, kijiji cha kihistoria cha Esfahak, kilicho katika mkoa wa Khorasan Kusini mwa Iran, mwaka jana (2024)kilitambuliwa kimataifa kwa kutajwa na Shirika la Utalii la Umoja wa Mataifa kuwa mojawapo ya Vijiji bora vya Utalii
Mabadiliko ya Esfahak kuwa kivutio cha kitamaduni na utalii wa kiikolojia yamepelekea kijiji hicho kupata Tuzo ya kifahari ya Usanifu wa Asia. Leo, kijiji hicho kinavutia watalii kutoka kote ulimwenguni kutokana na usanifu majengo wa kuvutia ambao umehifadhi utambulisho wa kitamaduni.