Rais wa Venezuela amesisitiza uungaji mkono kamili kwa haki za watu wa Palestina na haja ya kutekeleza haki dhidi ya jinai na vitendo vya mauaji ya kimbari.

Kwa mujibu wa Mtandao wa Al-Mayadeen, Rais wa Venezuela Nicolas Maduro ametangaza kwamba, amani ya kweli itapatikana tu wakati haki na uadilifu utakapotekelezwa dhidi ya uhalifu na vitendo vya mauaji ya kimbari.

Rais wa Venezuela aliendelea kusema kuwa, nchi yake inatangaza uungaji mkono wake usio na masharti kwa haki za watu wa Palestina na inatumai kuwa makubaliano ya kina na halali yanaweza kufikiwa ambayo yanadhamini haki za kisheria za watu wa Palestina.

Aidha amesisitiza kuwa, suala la Palestina ni suala takatifu zaidi na kwamba wananchi wa Palestina wana haki isiyopingika ya kuishi kwa amani na kuanzisha nchi huru.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, serikali ya Venezuela imepinga vikali mpango wa utawala wa Kizayuni wa Israel wa kuukalia kwa mabavu Ukanda wa Gaza na kuitaja hatua hiyo kuwa ni kuzidisha mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Palestina.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela, Yvan Eduardo Gil amesema kuwa, mpango huu wa kutaka kuikalia kwa mabavu Gaza unalenga kufuta uwepo wa watu wa Palestina na hauwezi kuvumiliwa na dhamiri ya ubinadamu.

Serikali ya Caracas imetaka kutiwa mbaroni mara moja viongozi husika wa Israel katika ngazi ya kisiasa, kiuchumi na  kidiplomasia na kuitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua kali na za haraka dhidi ya uamuzi wa Israel.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *