Tanzania yanufaika mradi wa bil 159/- sekta ya bahariTanzania yanufaika mradi wa bil 159/- sekta ya bahari

SERIKALI kupitia Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) imenufaika na mradi wa uchumi wa buluu na kituo cha mafunzo unaolenga kuimarisha rasilimaliwatu, teknolojia safi na ustawi wa jamii katika sekta ya bahari.

Mkuu wa DMI, Profesa Tumaini Gurumo alisema hayo alipowasilisha mradi huo wenye thamani ya Dola milioni 65.26 (Sh bilioni 159) wakati wa mkutano wa pembezoni mwa Mkutano wa 30 wa Umoja wa Mataifa wa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP 30) unaoendelea katika Jiji la Belem nchini Brazil.

Profesa Gurumo alisema matumizi ya boti za umeme yatapunguza gharama za uendeshaji kwa wavuvi kwa takribani asilimia 50 kutoka wastani wa Dola 12,800 hadi 6,400 kwa mwaka.

Alisema kupitia mradi huo, DMI itapata meli ya kisasa ya mafunzo yenye ukubwa wa 7,500 GT, kituo cha ubunifu na ujenzi wa boti za umeme na mtandao wa vituo 15 vya huduma baada ya mauzo na vituo vya kuchaji boti za umeme.

Profesa Gurumo alisema kwa kipindi cha miaka mitano, mradi unatarajiwa kutoa zaidi ya wataalamu 3,000 wa mabaharia, wahandisi na mafundi baharini na kupeleka boti 750 zenye injini za umeme na kupunguza hewa ya ukaa kwa zaidi ya asilimia 50 kutoka kwenye boti ndogo za kisasa.

Alisema utekelezaji wa mradi huo utasaidia kaya 100 kwa mwaka katika kilimo cha mwani na ufugaji wa viumbe baharini kwa njia rafiki kwa mazingira na kujenga uwezo kwenye jamii kupitia mafunzo ya teknolojia safi, utafiti na ubunifu.

Profesa Gurumo alisea mradi huo unaendana moja kwa moja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Sera ya Uchumi wa Buluu 2024, Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) 4, 8, 13 na 14 na malengo ya kupunguza uzalishaji wa kaboni katika sekta ya bahari.

Aidha, alisema uchumi wa buluu ni eneo lenye fursa kubwa ambazo hazijatumika na zikitumika ipasavyo zitakuwa ni uti wa mgongo wa mageuzi ya maendeleo ya taifa kutokana na kuwepo kwa maeneo makubwa ya vyanzo vya maji.

Ofisi ya Makamu wa Rais imeanzisha kitengo mahususi kwa ajili ya kuratibu uchumi wa buluu na pia Serikali ilizindua Sera ya Uchumi wa Buluu (2024) na mkakati wake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *