Marekani. Mwanamuziki wa R&B, R Kelly aliyewahi kutamba na ngoma kama I Believe I Can Fly, The World’s Greatest, Storm Is Over Now na nyinginezo ameeleza huzuni yake kubwa akiwa gerezani, akidai karibia mwaka sasa hakuna mtu wa familia yake aliyemtembelea. 

Katika maelezo yake yaliyochapishwa katika tovuti ya ‘ValidUpdates’ Kelly anasema moja ya jambo ambalo linamuumiza ni upweke. Hapo awali alikuwa msaada mkubwa kwa marafiki na ndugu kabla ya kuingia gerezani, lakini sasa anahisi uhusiano na watu hao umekwisha kwani anajiona kama yupo mwenyewe kwenye hii dunia.

Pamoja na maumivu hayo baadhi ya maofisa wanasema kwa sasa msanii huyo amekuwa karibu zaidi na Mungu, akiomba kama siku moja marafiki pamoja na ndugu watakwenda kumtembelea tena kama ambavyo walikuwa wakifanya pindi yupo uraiani.

Utakumbuka binti wa Kelly aitwaye Joanne ‘Buku Abi’ kupitia mahojiano yake ya hivi karibuni aliwahi kuweka wazi sababu ya kutomtembelea baba yake gerezani. Akidai uhusiano wake na baba yake ulishavunjika muda mrefu kutokana na makosa makubwa aliyohukumiwa.

Amesema licha ya kumpenda sana baba yake alipokuwa mdogo, maisha yalimgeuka baada ya kushuhudia madhara ya vitendo hivyo ndani ya familia.

Hata hivyo Joanne aliendelea kueleza kuwa hatothubutu kumpeleka mtoto wake gerezani kwani kunaweza kumsababishia matatizo ya kiafya na kisaikolojia. Amesema kuwa anataka mtoto wake akue kwenye mazingira mazuri na kwamba haoni sababu kuanzisha uhusiano kati ya mtoto na babu ambaye hawana uhusiano mzuri.

Aidha kwa upande wa mama yake Joanne, Drea, ameweka wazi kuwa ataendelea kusimamia uamuzi wa binti yake, kwani changamoto walizopitia kama familia ni kubwa, na kwamba athari za vitendo vya R. Kelly viliwavuruga sana watoto wake.

R. Kelly ambaye anatajwa kuwa nguli wa R&B alikamatwa mwaka 2019 na kuhukumiwa Juni 2022 kifungo cha miaka 30 jela kwa makosa ya unyang’anyi wa kingono, usafirishaji watu kwa ajili ya ngono (sex trafficking) na unyanyasaji wa watoto. 

Lakini Februari 2023 alihukumiwa kifungo cha miaka 20 kwa kesi ya picha za ngono za watoto (child pornography) lakini sehemu kubwa ya adhabu hiyo inaendeshwa sambamba, hivyo kwa ujumla anasalia kutumikia miaka 30.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *