
Dar es Salaam. Mchekeshaji maarufu kutoka kundi la Watubaki, Raulenc Minja maarufu kama Kipotoshi, amemtaja marehemu MC Pilipili kama Mfalme wa uchekeshaji nchini. Amesema wengi katika sanaa ya vichekesho walimchukulia kama mzazi na mlezi wao wa kisanaa.
Kipotoshi ameyasema hayo, alipowasili nyumbani kwao marehemu eneo la Swaswa jijini Dodoma, ambako shughuli za maombolezo zinaendelea.
“Pilipili alikuwa mwamba, tulimwona kama mzazi kwenye sanaa, mtu wa kushauri na kuinua wengine,”amesema
Hata hivyo, Kipotoshi hakuficha machungu yake juu ya namna msanii huyo alivyofariki. Ametoa wito kwa jamii kuziachia mamlaka kufanya uchunguzi kamili ili ukweli ujulikane bila kukurupuka na taarifa zisizo na msingi.
Mbali na Kipotoshi naye mwanamuziki Sunday Mjeda (Linex) ameeleza majonzi yake akisema Pilipili hakuwa tu msanii wa vichekesho, bali alikuwa mtu mwenye kugusa maisha ya wengine kwa kuwatafutia fursa na kazi.
Amesema MC Pilipili alikuwa kama daraja la kipato kwa wasanii wengi, hususani wale wanaoimba katika sherehe mbalimbali, ikiwamo harusi.
“MC Pilipili alikuwa mgawa riziki, Unajua mimi nina nyimbo zinazopendwa kwenye maharusi, na mara nyingi hata kama sina kazi wikiendi. Anaweza kunipigia na kuniuliza kama nina suti nzuri, kisha ananiambia nije nifanye kazi,” amesema Linex.
Ameongeza kuwa kupitia mwaliko wa Pilipili aliweza kujipatia kipato na kuendeleza maisha, jambo analoliona kama alama ya upendo na kujali kwa marehemu. Linex amesema tasnia ya burudani imepata pigo kubwa, akisisitiza kuwa mchango wa MC Pilipili utaendelea kukumbukwa na wengi waliowahi kuguswa na moyo wake wa kutoa fursa.
Licha ya wengi kumuona Pilipili kama msanii, mwanamuziki Mon Centrozone amezungumza namna ambavyo anamkumbuka Mc pilipili na kusema kuwa alikuwa mwalimu wake wa Civics kipindi akiwa kidato cha nne.
Amesema kuwa katika vitu anavyovikumbuka kutoka kwake ni umahili wake katika kufundisha somo la Uraia (Civics) kwani kutokana na umahili wake usingeweza kukosa kipindi chake.