Jumanne huko Belém, mawaziri kutoka Colombia, Ujerumani, Kenya, Visiwa vya Marshall, Sierra Leone, Uingereza na nchi nyingine kadhaa walitoa uungwaji mkono mkubwa kwa pendekezo la Brazil la kuinua suala hilo katika majadiliano ya mwaka huu ya Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi.

Muungano huo umetaka majadiliano kuimarisha lugha kuhusu mabadiliko kutoka kwa matumizi ya mafuta ya kisukuku katika rasimu ya maandishi yanayotarajiwa kuidhinishwa leo Jumatano.

Lengo lao ni kuharakisha hatua na kuweka ongezeko la joto duniani ndani ya kiwango cha kilichoidhinishwa cha nyuzijoto1.5°C.

Kisha ukimya ukatawala. Mawaziri wakamsikiliza Balozi wa Vijana wa COP30, Marcele Oliveira, alipokwenda mbele akiwa amebeba dharura ya kizazi kizima.

“Mafuta ya kisukuku yanaharibu ndoto,” ameonya, akisema mabadiliko kutoka kwenye nishati hizo ni “harakati muhimu zaidi ya haki ya tabianchi ya kizazi hiki.”

Bingwa wa Hali ya Hewa kwa Vijana wa COP30, Marcele Oliveira, akizungumza katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi unaoendelea huko Belém, Brazil.

© UNFCCC/Zô Guimarães

Bingwa wa Hali ya Hewa kwa Vijana wa COP30, Marcele Oliveira, akizungumza katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi unaoendelea huko Belém, Brazil.

Kulinda mustakbali

Akizungumza na UN News, Bi. Oliveira amesisitiza kuwa watoto na vijana lazima wawe kiini cha kila majadiliano ya COP30.

“Tulipata uamuzi kutoka Mahakama ya Kimataifa ya Haki ukisema kwamba kutokuchukua hatua kwa nchi kuhusu mabadiliko ya tabianchi ni uhalifu wa kimazingira. Hivyo basi, tunahitaji kushinikiza nchi zichukue maamuzi bora kuhusu tabianchi, na hili pia ni kipaumbele,” amesisitiza.

Bi. Oliveira  ameongeza kuwa “Bila shaka, tunahitaji kuachana na mafuta ya kisukuku, kuwekeza katika ulinzi wa misitu, na kuwalinda wale wanaoilinda. Na bila shaka, kwa vijana, kutambuliwa kwa hatua za pamoja katika ngazi ya jamii, zinazoongozwa na vijana, ni jambo muhimu sana.”

Washiriki wakati wa mazungumzo ya Vijana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika COP30 huko Belém, Brazil.

© UNFCCC/Kiara Worth

Washiriki wakati wa mazungumzo ya Vijana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika COP30 huko Belém, Brazil.

Guterres: Vita ya uamuzi

Baadaye siku hiyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alikutana na wajumbe wa vijana na kuomba radhi, samahani iliyobeba utambuzi mzito. Vizazi vilivyotangulia, amesema, vimeshindwa kudhibiti mgogoro wa tabianchi. Makadirio ya kisayansi yanathibitisha kuwa joto litapita kiwango cha nyuzi joto 1.5°C.

Sasa, amewasihi vijana kusimama pamoja naye katika kile alichoita “vita ya uamuzi kuhakikisha kupita kwa kiwango hicho kunakuwa kwa muda mfupi iwezekanavyo.

Amesisitiza kuwa mabadiliko kutoka mafuta ya kisukuku kwenda nishati mbadala ni muhimu, na yanahitaji kukabiliana na makundi yenye nguvu ya ushawishi ambayo “yanatanguliza faida kuliko ustawi wa jumuiya ya kimataifa na sayari.” Shinikizo la vijana, amesema, ni muhimu katika COP30.

Tunataka tu kuwa watoto!

João Victor da Silva, mwenye umri wa miaka 16 kutoka Brazil, amemwambia kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa “Hatupendi kuwa wanaharakati, tunataka tu kuwa watoto na vijana balehe, lakini kwa bahati mbaya watu wazima hawafanyi maamuzi sahihi.”

Kutoka Aruba, Nigel Maduro ameshiriki ukweli mchungu, fukwe alikojifunzia kuogelea zinatoweka. Ameonya kuwa majadiliano yanakwenda polepole  labda polepole kupita kiasi kwa taifa lake la kisiwa, linalokabiliwa na joto kali na kuongezeka kwa kina cha bahari.

Vijana kutoka nchi kadhaa wamerudia ombi lile lile”chukueni hatua sasa ili kulinda mustakabali unaoweza kutoweka”.

Katibu Mkuu amekubali kwamba ushirikishwaji mkubwa wa vijana hasa kutoka jamii za watu wa asili unaweza kuleta matokeo bora zaidi.

Amekiri pia wito wa ufadhili wa moja kwa moja na usio na urasimu kwa jamii za watu wa asili, na akaahidi kuboresha mazingira ya kufanya hilo liwezekane.

Watoto wanapaza sauti zao katika mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Hali ya Hewa mjini Belém, Brazili.

© UNFCCC/Zô Guimarães

Watoto wanapaza sauti zao katika mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Hali ya Hewa mjini Belém, Brazili.

Mikutano ya vijana ndiyo inaleta matumaini

Kiongozi wa jamii za watu wa asili Txai Suruí, ameeleza mkutano wa vijana kuwa ni moja ya matukio yanayotia moyo zaidi ya COP30.

Lakini ameonya kuwa msitu wa Amazon uko hatarini sana kufikia hatua ya kuporomoka kuelekea hali ya jangwa.

“Maandamano ndiyo yanayotofautisha COP hii, kwa sababu ingawa baadhi ya nchi huenda hazipendi, Brazil ni nchi ya kidemokrasia, na maandamano pia hutumika kuhakikisha viongozi hawa wanachukua maamuzi yanayolinda uhai.”

Bi. Txai amebainisha kuwa ushawishi wa makampuni makubwa bado ni mkubwa kuliko ujumbe wote pamoja na hakika mkubwa kuliko uwakilishi wa jamii za watu wa asili hali inayosababisha kutokuwepo kwa uwiano wa sauti. Hata hivyo, anaona ongezeko la utambuzi kwamba jamii za watu wa asili ni walinzi wa mazingira.

Mabadiliko ya haki

Wakati huohuo, kwa Bi. Oliveira, mabadiliko kutoka matumizi ya mafuta ya kisukuku lazima yawe ya haki mtazamo unao“isikiliza, kuikaribisha na kuisikia ardhi na jamii.”

Hatua kama kutenga na kulinda ardhi za watu wa asili, amesema, ni muhimu ili kuhakikisha mabadiliko haya hayawaumizi zaidi watu ambao tayari wameathirika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *