Wawakilishi kutoka zaidi ya nchi 90, pamoja na viongozi wa kidini, wasomi na watu mashuhuri kutoka kote duniani, wametangaza utayarifu wao wa kuhudhuria mazishi ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Jumanne, Ali Akbar Pourjamshidian, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran anayeshughulikia masuala ya Usalama na katibu wa kamati ya maandalizi ya mazishi, amesema kwamba zaidi ya nchi 30 tayari zimewasilisha maombi rasmi ya kutuma wajumbe wa ngazi za juu kwenye mazishi hayo.

Pourjamshidian ameendelea kusema kuwa mazishi hayo yaliahirishwa ili kutoa muda wa kutosha wa kuandaa shughuli kubwa ya kitaifa na kimataifa.

Pia ameeleza kuwa, kwa mujibu wa maamuzi ya ofisi ya marehemu kiongozi na mwongozo wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei, shughuli hiyo itafanyika kwa siku kadhaa.

Afisa huyo amesema matukio hayo yamepangwa chini ya usimamizi wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa, Ofisi ya Kiongozi Muadhamu na makao makuu ya kitaifa yaliyoanzishwa na utawala chini ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Mohammad Reza Aref.

Shughuli ya mazishi na kuaga mwili wa Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu zitafanyika Tehran, Qum, Mash’had na katika miji mitakatifu ya Iraq.

Pourjamshidian amesema Iraq imeunda kamati ya kitaifa ya maandalizi ya mazishi inayoongozwa na Ofisi ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo kufuatia uratibu mpana kati ya maafisa wa Iran na Iraq, ikiwa ni pamoja na mikutano iliyohudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Sayyid Abbas Araqchi na Rais, Waziri Wakuu wa Iraq na maafisa wengine wa ngazi za juu wa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa, mwili wa Ayatullah Ali Khamenei utapelekwa Iraq mnamo Julai 8, ambapo mapokezi rasmi yanatarajiwa kufanyika katika uwanja wa ndege wa Baghdad au Najaf yakishirikisha maafisa wakuu wa Iraq. Shughuli ya mazishi imepangwa kufanyika katika miji mitakatifu ya Najaf na Karbala.

Siku inayofuata, Julai 9, Swala ya Maiti na mazishi yamepangwa kufanyika katika mji mtakatifu wa Mash’had, ambapo kiongozi aliyeuawa shahidi wa Iran na familia yake wanatarajiwa kuzikwa karibu na Haram ya mjukuu wa Mtume wetu Muhammad (SAW), Imam Reza (AS).

Ameongeza kuwa ushiriki mpana wa watu kutoka nchi za Kiislamu, ikiwa ni pamoja na Iraq, Pakistan, Afghanistan na nchi nyingine jirani, unatarajiwa kuimarisha zaidi mshikamano katika Umma wa Kiislamu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *