BAADA ya mapumziko ya ligi kupisha mechi za timu za taifa, Ligi Kuu Bara inaendelea tena leo kwa mechi mbili kupigwa, ambapo KMC inayoburuza mkiani, itakuwa na kibarua cha kupambana na JKT Tanzania, huku Namungo ‘Wauaji wa Kusini’ wakiikaribisha Dodoma Jiji.

Mechi hiyo ya KMC itakayochezwa saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa KMC Mwenge jijini Dar es Salaam, inazikutanisha timu zote ambazo zimekuwa na mwenendo usioridhisha tangu msimu umeanza, huku zaidi ikiwa ni kikosi hicho cha Kinondoni.

Katika mechi sita ilizocheza KMC msimu huu, tayari imepoteza tano mfululizo, huku ikishinda moja iliyokuwa ya ufunguzi dhidi ya Dodoma Jiji kwa bao 1-0, Septemba 17, 2025, jambo linalochochea presha zaidi kwa kocha Mbrazil Marcio Maximo.

KMC ilichapwa bao 1-0 na Singida Black Stars na maafande wa Tanzania Prisons, pia ikachapwa mabao 3-0 na Mbeya City, ikakumbana na kichapo tena cha 1-0 kutoka kwa Fountain Gate, kisha mechi ya mwisho na ya tano ikacharazwa na Yanga 4-1.

Kwa upande wa maafande wa JKT Tanzania, hawajashinda mechi nne mfululizo za Ligi Kuu Bara kati ya sita walizocheza msimu huu, tangu mara ya mwisho waliposhinda mabao 2-1, dhidi ya Coastal Union, kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga, Septemba 22, 2025.

LIG 01

Mechi ya Tanga ndiyo ya ushindi kwa JKT Tanzania msimu huu, baada ya kutoka sare nne ikianza na ya kufungana bao 1-1, dhidi ya Mashujaa, Azam na Namungo, kisha 2-2 na Mbeya City, huku ikipoteza moja nyumbani 2-1 dhidi ya Simba.

Mara ya mwisho kwa timu hizo kukutana, ilikuwa kwenye Uwanja wa KMC, Februari 18, 2025, ambako JKT ilishinda kwa mabao 2-0, yaliyofungwa na Hassan Nassor dakika ya 10 na aliyekuwa kipa wa KMC, Wilbol Maseke aliyejifunga katika dakika ya 67. 

Katika mechi ya mwisho itakayopigwa leo kwenye Uwanja wa Majaliwa Lindi saa 1:00 usiku, Namungo iliyocheza mechi nne mfululizo bila ya ushindi tangu mara ya mwisho ilipoifunga Tanzania Prisons kwa bao 1-0, Septemba 21, 2025, itaikaribisha Dodoma Jiji.

LIG 02

Namungo iliyocheza mechi sita msimu huu, imeshinda moja tu, ikitoka sare tatu na kuchapwa mbili, huku kwa upande wa kikosi cha Dodoma Jiji kikishinda moja tu, sare mbili na kupoteza tatu, kikiwa hakina mwendelezo mzuri pia.

Mechi ya mwisho kati ya timu hizo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Majaliwa, zilitoka sare ya mabao 2-2, Februari 9, 2025, ambapo ya Namungo yalifungwa na Pius Buswita na Erasto Nyoni, huku ya Dodoma yakifungwa na Paul Peter na Apollo Otieno. 

Kocha wa Namungo, Juma Mgunda amesema shida aliyokuwa anaifanyia kazi ni kutengeneza balansi katika eneo la kujilinda na la ushambuliaji, huku Amani Josiah wa Dodoma Jiji akiwataka nyota wa kikosi hicho kutumia vizuri nafasi wanazotengeneza.

MSIKIE BAJANA

Kiungo wa JKT Tanzania, Sospeter Bajana amekiri mechi ya leo dhidi ya KMC, haitakuwa rahisi licha ya kwamba amejipanga vilivyo.

Bajana aliye JKT msimu huu akitokea Azam FC akisaini mkataba wa mwaka mmoja amesema, wachezaji waliokuwa kambini tangu Jumatatu, wamejipanga kwa mechi hiyo ili kuzoa pointi tatu.

LIG 03

“Unajua KMC imeanza msimu vibaya, hivyo hii mechi wataitumia kusafisha njia ndio maana nasema haitakuwa rahisi kuwakabili. Kwa muda huu wa mapumziko tumejiweka katika hali nzuri kwa kufanya mazoezi zaidi, lakini naamini wapinzani nao hawakulala,” amesema Bajana na kuongeza; “Msimu huu sitaki kulegeza kamba, kama ulivyoona nimerejea uwanjani, hivyo sitarudi nyuma hapa ni kasi tu na hilo nalipambania kuanzia mazoezini na juhudi binafsi.”

Bajana alicheza mechi ya mwisho dhidi ya Simba ambapo maafande hao walilala kwa mabao 2-1.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *