
Dar es Salaam. Baada ya wimbo wa Pawa kutoka kwa Mbosso kufanya vizuri kwenye majukwaa mbalimbali ya muziki, mkali huyo wa kuandika mashairi ya mapenzi ametangaza kuachia remix tatu.
Ngoma hiyo inapatikana kwenye EP yake ya ‘Room Number 3’ yenye nyimbo saba ikiwamo Aviola, Nusu Saa, Siko Single, Merijaan, Tena na Asumani. Tangu aiachie Juni 2025 ikiwa ni miezi mitano imepita, imepokelewa vizuri.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Mbosso ameweka chapisho la kava tatu za remix hizo ambazo atafanya na mastaa kutoka Kenya, Rwanda na Tanzania huku akisindikizia na ujumbe uliosomeka: “Leo Saa Sita Usiku 😂.”
Kava ya kwanza ameweka picha na wasanii kutoka Kenya akimaanisha kufanya na Bien pamoja na rapa Khaligraph Jones, Rwanda akipiga na The Ben huku Bongo akiwashirikisha Billnass, Darassa na GNako.
Wimbo wa Pawa tangu kuachiwa kwake Juni 2025, umefanya vizuri huku ukishika chati za juu katika mataifa mbalimbali pamoja na kuweka rekodi ya kufikisha watazamaji zaidi ya milioni 30 kwenye mtandao wa YouTube ndani ya kipindi kifupi cha miezi miwili tu tangu uingie sokoni.
Mpaka kufikia sasa, video ya wimbo huo imetazamwa zaidi ya mara milioni 46 katika mtandao wa YouTube. Remix hizo tatu zote kwa pamoja zinatarajia kutoka usiku wa leo Alhamisi Novemba 20, 2025.