Katika mahame ya mitaa ya Khartoum, watu wanajaribu kurejea kwenye kile kinachoonekana kama magofu. Nyumba, shule, na vituo vya afya vyote vimeporomoka. Miongoni mwao ni Sittana, akitembea kupita vifusi vya nyumba yake iliyosambaratishwa
 

Mtoto wake wa miezi saba, Ali, ni amekonda kupita kiasi kutokana na utapiamlo mkali anasema

“Nilianguka shimoni na nilitokwa damu kila mahali. Askari wa RSF walifyatua risasi kwa watoto wangu lakini ziliwakosa. Niliwaokoa, lakini mwanangu Ali alizaliwa na uzito mdogo sana. Wakati wa ujauzito sikuwa nakula vizuri. Hakukuwa na chakula, maji yalikuwa ya chumvi. Hakukuwa na chakula popote.”
Katika jimbo la Darfur, hali ni mbaya zaidi. Huko Tawila, WFP inagawa chakula kwa zaidi ya watu 100,000 waliokimbia machafuko ya hivi karibuni El Fasher, ikiwa ni sehemu ya msaada wake kwa takribani watu milioni moja katika eneo hilo.
 

Familia zinapokea mgao wa mwezi mmoja ambao ni nafaka, kunde, mafuta na chumvi pamoja na virutubisho kwa watoto na wanawake wajawazito au wanaonyonyesha.

Angham, aliyekimbia El Fasher na watoto wake wawili ni miongoni mwa wanaopokea msaada anasema  “Tukipata msaada tunaweza kula, lakini tunahitaji mablanketi na sweta ili kuhimili baridi hii na magonjwa.”
Kutoka makao makuu ya WFP mjini Rome Italia, mratibu wa dharura Shaun Hughes anasema changamoto zinazidi kuongezeka.

“Tunazo changamoto mbili kuu, hasa katika maeneo yanayokumbwa zaidi na mgogoro, majimbo ya Darfur na Kordofan. Kwanza ni ufikiaji, hasa katika miji kama Al-Fasheh na Kadugli. Pili ni rasilimali. Tunawafikia watu milioni nne hadi tano kila mwezi, lakini wengi wanapata mgao mdogo. Na kufikia Januari, hatutakuwa na rasilimali za kuendelea kutoa kiwango hiki cha msaada.”
 

Huko Kadugli, ambako njaa ilithibitishwa Oktoba, msafara wa pamoja wa Umoja wa Mataifa umewasili kwa mara ya kwanza tangu vita kuanza ukiwa na chakula, maji na vifaa vya afya. Lakini mashirika ya misaada yanaonya bila misafara ya mara kwa mara, njaa inaweza kuenea.

WFP inasema inahitaji ufadhili wa haraka na njia salama za kufikisha misaada ili kuzuia njaa isiangamize mamilioni ya watu nchini Sudan.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *