Dar es Salaam. Ukuaji wa sekta ya miundombinu na uzalishaji wa bidhaa za ujenzi umetajwa kuchochea ongezeko la uchimbaji wa madini ya ujenzi na viwandani, hatua iliyofanya thamani ya sekta hiyo kufikia zaidi ya Sh1 trilioni katika mwaka wa fedha 2024/2025.

Ukuaji huo unatokea wakati Tanzania ikiendelea kushuhudia ongezeko la miradi ya ujenzi inayosajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), sambamba na upanuzi wa miundombinu ya usafirishaji, usafiri na ujenzi wa nyumba za makazi, ambavyo kwa pamoja vimeboresha mahitaji ya bidhaa zinazotokana na madini ya ujenzi.

Akizungumza katika hafla ya usiku wa Tuzo za Afrika Mashariki za Sekta ya Ujenzi na Miundombinu (EABC) iliyofanyika Ijumaa, Novemba 28, 2025, Naibu Waziri wa Madini, Dk Steven Kiruswa, alisema ukuaji huo umeongeza mapato yanayoingia moja kwa moja kwenye mzunguko wa uchumi na hivyo kuchochea maendeleo ya taifa.

Tuzo hizo zimetolewa kwa lengo la kutambua kampuni zinazofanya vizuri katika sekta ya madini hususan watoa huduma mbalimbali ikiwemo chakula, vifaa vya ujenzi, malazi, nishati, usafirishaji na huduma za kifedha.

“Mnaweza kuona ni kwa kiwango gani sekta ya madini inavyochangia bidhaa muhimu katika ujenzi wa miundombinu na jinsi mnyororo wa thamani unavyozidi kupanuka,” alisema Dk Kiruswa.

Hata hivyo, licha ya mchango mkubwa wa sekta hiyo, Dk Kiruswa aliwataka wadau wa ujenzi kuzingatia utunzaji wa mazingira na kuendelea kutumia teknolojia za kisasa katika shughuli zao.

Alisisitiza kuwa kila mchimbaji, awe mdogo au mkubwa, lazima awasilishe taarifa ya tathmini ya athari kwa mazingira kabla ya kuanza uchimbaji.

“Hii taarifa itaonyesha baada ya kumaliza uchimbaji, mgodi utaachwa katika hali gani na hatua gani zitachukuliwa kurejesha mazingira katika ubora wake. Ndiyo maana leo ukienda Nyanzaga, utaliona eneo lililowekwa katika hali nzuri baada ya uchimbaji,” aliongeza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chemba ya Ujenzi, Pamela Shoo, alisema sekta ya ujenzi na miundombinu ni nguzo muhimu katika ukuzaji wa uchumi, hivyo aliitaka Serikali kuendelea kuimarisha ushirikiano na wadau ili kuiwezesha sekta hiyo kuendana na kasi ya maendeleo ya kiteknolojia duniani.

Gerald Tronche, mmoja wa walioshinda tuzo katika kipengele cha mtoa huduma bora wa chakula kutoka Gwambina Group, alisema kampuni yake imeshinda tuzo hiyo kwa mara ya pili, hatua ambayo imewahamasisha kuendelea kuboresha huduma zao.

Tronche, ambaye ni meneja masoko wa kampuni hiyo, alisema Gwambina Group imekuwa ikitoa huduma za chakula katika miradi mikubwa ya Serikali na sekta binafsi, hali iliyowafanya watambulike kwa ubora wa kazi yao.

“Tunajivunia kutoa huduma bora na kujibu changamoto ndani ya saa 24. Pia tuna wafanyakazi wenye uzoefu mkubwa, baadhi yao wakiwa na zaidi ya miaka 30 kwenye tasnia hii. Tuna uwezo wa kushindana na kampuni yoyote duniani kutokana na viwango vyetu,” alisema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *