Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres kupitia ujumbe wake maalum kwa siku hii anasema dunia imepiga hatua kubwa katika vita dhidi ya ukimwi lakini sasa hatua hizo ziko hatarini.

“Maendeleo tuliyopata hayawezi kukanushwa. Tangu mwaka 2010, maambukizi mapya yameshuka kwa asilimia 40, na vifo vitokanavyo na UKIMWI vimeshuka zaidi ya nusu na fursa ya matibabu ni bora kuliko awali.”

Lakini Guterres anasema mamilioni ya watu bado wanaachwa nyuma wakinyimwa kinga na matibabu ya kuokoa maisha kutokana na ukosefu wa usawa, unyanyapaa au mahali wanakoishi.

“Mamilioni bado hawana huduma za kinga na matibabu ya VVU kwa sababu ya wao ni kina nani, wanaishi wapi, au unyanyapaa wanaokumbana nao.”

Na kutokana na kupungua kwa ufadhili, huduma zilizokatizwa na kuongezeka kwa sheria kandamizi, Umoja wa Mataifa unaonya kwamba mafanikio yaliyodumu kwa miongo kadhaa sasa yako hatarini kuporomoka.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa  linalohusika na masuala ya Ukimwi UNAIDS Winnie Byanyima amesema mwaka 2025 umeleta mgogoro mkubwa wa ufadhili unaotishia kuyumba kwa mafanikio yaliyofikiwa kwa juhudi kubwa akisisitiza kuwa“Wakati wa mgogoro, dunia lazima ichague mabadiliko badala ya kurudi nyuma. Kwa pamoja, bado tunaweza kumaliza UKIMWI ifikapo 2030 tukichukua hatua kwa haraka, umoja na kujitolea kusikoyumba.”

Anasema mashirika yanayoongozwa na jamii ambayo ni muhimu kufikia watu walio pembezoni ndiyo yanayoumia zaidi kwa kupunguzwa kwa ufadhili wa fedha.
Pia amesema sheria kandamizi zinazidisha ugumu wa kupata huduma, wakati ambapo huduma hizo zinahitajika zaidi. Amesisitiza kuwa dunia lazima ilinde haki na kuondoa vikwazo vinavyochangia maambukizi mapya.

“Uongozi wa kisiasa ni muhimu sana. Tunahitaji suluhu za kubadilisha mfumo, zinazokomesha unyanyapaa na ubaguzi milele, na kulinda haki za wanawake, wasichana na watu wa LGBTQ+.”Amesisitiza

Licha ya changamoto, viongozi hao wanasema bado kuna fursa ya kumaliza janga la UKIMWI lakini ni lazima pawepo na uwekezaji mpya na mshikamano wa kimataifa.

“Kumaliza UKIMWI kama tishio la kiafya kufikia 2030 kunawezekana. Hebu tukamilishe kazi hii.”

Siku hii ya UKIMWI Duniani inakumbusha kuwa dunia ina nyenzo za kutokomeza janga hili, iwapo tu itaamua kuzitumia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *